Vyombo vya habari vya Iraq na duru za kijeshi nchini humo zimeripoti kuwa, kambi ya kijeshi ya Marekani katika mji wa Erbil, makao makuu ya eneo la Kurdistan la Iraq imeshambuliwa kwa makombora ya balestiki.
Kadhalika ripoti hiyo imeeleza kuwa, kambi mbili za kutoa mafunzo za Shirika la Kijasusi la Utawala wa Kizayuni wa Israel (MOSSAD) zimeshambuliwa pia kwa makombora ya balestiki katika eneo hilo la Erbil, kaskazini mwa Iraq.
Duru za kiintelijensia za eneo la Kurdistan zinaarifu kuwa, makombora 12 ya balestiki yametumika katika shambulio hilo la alfajiri ya leo katika mji wa Erbil.
Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kupambana na Ugaidi ya Kurdistan imenukuliwa na vyombo vya habari ikisema kuwa, makombora hayo yaliyopiga Erbil yamevurumishwa kutoka nje ya Iraq.
Habari zaidi zinaarifu kuwa, ubalozi mdogo wa Marekani uliokuwa ukiendelea kujengwa katika eneo hilo lenye mamlaka ya ndani la Iraq umeshambuliwa pia kwenye shambulio hilo la makombora ya balestiki.
Taharuki imetanda katika eneo la Kurdistan, huku barabara za kuelekea katika uwanja wa ndege wa Erbil zikifungwa. Maafisa wa Marekani wamekiri kutokea mashambulio hayo, lakini wanadai kuwa hakuna majeruhi wala vifo.
Inaarifiwa kuwa, sauti za ving'ora zimesikika katika ubalozi wa Marekani ulioko kwenye eneo lenye ulinzi mkali la 'Green Zone' katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad.