Kesi kutishia kuua kwa bastola kuanza Aprili 7



KESI ya kutishia kuua kwa bastola inayomkabili mfanyabiashara wa Kariakoo, Adelard Lyakurwa, inatarajia kuanza kusikilizwa Aprili 7, mwaka huu.

mfanyabiashara wa Kariakoo, Adelard Lyakurwa (katikati) akiingia mahakamani. (picha maktaba)
Kesi hiyo ilipaswa kuanza kusikilizwa jana katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala mbele ya Hakimu Mkazi Laizer Confort, lakini ilikwama kwasababu hakimu huyo alikuwa na udhuru.

Ilidaiwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Nestori Baro, aliyeahirisha kwa niaba na kusema kuwa hakimu anayesikiliza kesi hiyo ana udhuru na shauri liliahirishwa hadi tarehe iliyopangwa kwa ajili ya kuanza kusikiliza mashahidi wa upande wa mashtaka.

Katika kesi hiyo, Lyakurwa anashtakiwa kwa kumtishia kumuua kwa bastola mfanyabiashara maarufu Valence Lekule.

Mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 89 (2)(a) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019.


 
Inadaiwa katika maelezo ya awali kwamba Julai 30, 2020 maeneo ya Kariakoo, mtaa wa Mbaruku na Swahili, Wilaya ya Ilala mshtakiwa akiwa na lengo la kuua, alimtishia Lekule kumuua kwa kutumia bastola huku akijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Mshtakiwa anadaiwa kuwa ni mkazi wa Msasani na siku ya tukio la kutishia kuua alikamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi cha Kati kwa tuhuma za kutishia kuua.

Mshtakiwa alikana maelezo yote kuhusu tuhuma zake, lakini alikubali kwamba tarehe iliyotajwa alikuwa maeneo ya Kariakoo, mtaa wa Mbaruku na Swahili na Mei 12, mwaka huu, alikamatwa na kufikishwa mahakamani.


Upande wa Jamhuri katika kesi hiyo unatarajia kuita mashahidi saba.

Mshtakiwa yuko nje kwa dhamana yenye masharti ya kuwa na wadhamini wawili waliokuwa na barua zinazotambulika kisheria na walisaini dhamana ya maandishi ya shilingi milioni moja.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad