Aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya akiwa na baadhi ya washitakiwa wenzake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kabla kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili kuahirishwa leo Alhamisi Machi 10,2022. Picha na Janeth Mushi
Arusha. Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita imekwama kuendelea kusikilizwa kutokana na Hakimu anayeisikiliza kuwa na majukumu mengine ya kiofisi.
Leo Alhamisi Machi 10, 2022, Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ilipanga kuendelea kusikiliza shauri hilo namba 27/2021 kwa shahidi wa tano wa utetezi ambaye pia ni mshitakiwa wa sita, Jackson Macha (30) kuendelea kujitetea.
Akiahirisha kesi hiyo, Hakimu Mkazi Pamela Meena alieleza kuwa Hakimu Mkazi Mwandamizi Patricia Kisinda, anayesikiliza shauri hilo bado anaendelea na majukumu ya kiofisi hataweza kuendelea kulisikiliza hadi Jumatatu Machi 14, 2022.
"Hakimu bado anaendelea na majukumu ya kiofisi hataweza kuendelea kusikiliza shauri hili kwa hiyo kesi itaendelea kusikilizwa Jumatatu,"amesema
Mahakama hiyo leo ilipanga kutoa uamuzi mdogo kufuatia maombi ya mshitakiwa wa tatu Watson Mwahomange, ambaye alishindwa kujitetea jana baada ya mawakili wanaowatetea washitakiwa wengine kuweka pingamizi kuzuia mahakama kutoa amri kwa Takukuru kumpatia simu yake aitumie kujitetea.
Jana Mwahomange aliomba mahakama iamuru Takukuru walete simu yake mahakamani hapo ili atumie kama kielelezo. Bonyeza hapa kusoma kilichojiri mahakamani jana