Kiama Cha Wezi wa Fedha za Umma




Arusha. Katika kuongeza uwajibikaji, Serikali imetangaza kuwachukulia hatua kali watumishi wa umma wanaochezea fedha za miradi ya maendeleo.

Onyo hilo limetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alipozungumzia mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan madarakani, akisisitiza kuwa hakuna mradi utakaosimama kutokana na uzembe wa mtu mmoja au kikundi kidogo kinachousimamia.

“Watakaokiuka utaratibu uliowekwa, wataendelea kunyofolewa serikalini na tayari hatua zimeshaanza kuchukuliwa na zitaendelea kuchukuliwa,” alisema Dk Mwigulu.

Hatua za sasa, alisema zitahusisha za kinidhamu na kisheria kwa watu wanaokwamisha miradi inayowalenga wananchi wengi, badala yake wanazikwepesha fedha zilizotengwa kwa manufaa binafsi.


Tofauti na ilivyokuwa mwanzo, kwamba mtumishi aliyebainika kuhusika na upotevu wa fedha za umma alikuwa anaondolewa kwenye nafasi yake lakini mshahara wake hauguswi, alisema Serikali inakusudia kubadilisha sheria ili kila anayeharibu awe anajipunguzia na mshahara wake pia.

“Tegeni macho na masikio yenu, mtawaona. Wataondolewa mmojammoja. Wapo waliokuwa wanaondolewa kwenye vyeo baada ya kuvurunda mambo lakini wanaendelea kulipwa mishahara ya awali, sheria hiyo inafanyiwa kazi ili kuwaadhibu kadri inavyotakiwa.

KIAMA PIC
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba akisalimiana na baadhi ya viongozi wa wizara hiyo wakati akiwasili kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu mafanikio ya awamu ya sita, jijini Arusha juzi. Picha WFU
Hatua za kisheria na kinidhamu zitaendelea kuchukuliwa kwa watu wote watakaofanya uzembe katika usimamizi wa fedha za umma,” alisema.


Wengine walioonywa katika utekelezaji wa majukumu yao, waziri alisema ni wale wanaoisababishia halmashauri kupata hati chafu ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) lakini ilikuwa ikiadhibiwa halmashauri kwa kupunguziwa fedha za maendeleo, lakini mabadiliko yanayokuja yatawagusa waliosababisha hali hiyo huku miradi ya wananchi ikiendelea kutekelezwa.

Hata halmashauri ambazo zilikuwa zinapelekewa fedha za miradi lakini hazizitumii na mwisho wa siku zinazirudisha Hazina, alisema watendaji wakae macho kwa kuwa pia wataondolewa.

“Popote utakapobainika mchezo mchafu, Wizara ya Fedha na Tamisemi tunashirikiana kuandaa ripoti na kutoa mapendekezo ya hatua za kuwachukulia watu wanaohusika katika udanganyifu huo. Rais amesema watakaosababisha uchafu ndio watakaoondoka,” alisema Dk Mwigulu.

Matokeo chanya

Kuhusu utendaji wa Serikali kwa mwaka mmoja uliopita, Dk Mwiguli alisema hatua za kisera zilizochukuliwa zimekuwa na matokeo mazuri yaliyosaidia kuimarisha sekta ya fedha nchini.


Licha ya changamoto ya janga la Uviko-19 na vita vilivyoathiri uchumi wa dunia, alisema mikopo chechefu ilipungua kutoka wastani wa asilimia nane mpaka asilimia tatu kutokana na uamuzi wa Serikali kulipa madeni ya wazabuni, makandarasi na watoa huduma kwenye taasisi za umma.

Ulipaji wa madeni hayo, alisema umewawezesha wengi kulipa mikopo benki na wafanyabiashara walikochukua malighafi za kutekeleza miradi waliyoshinda zabuni.

Pamoja na hilo, alisema mzunguko wa fedha umeongezeka kwa asilimia 9.2 kutokana na mambo kadhaa yaliyofanywa, ukiwamo mkopo wa Sh1.3 trilioni kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) zilizotumika kujenga shule 12,000 kwa kuwatumia makandarasi wa ndani.

Mpaka Februari, alisema Serikali ilikusanya Sh15.9 trilioni kutoka vyanzo vya ndani, sawa na asilimia 93 ya matarajio, hivyo kuiwezesha kutekeleza miradi ya maendeleo na ile ya kimkakati.


Waziri pia alizungumzia kasi ya ongezeko la mfumuko wa bei kwamba unasababishwa na vitu vilivyo nje ya udhibiti wa Serikali na unaigusa dunia nzima, hivyo kupandisha gharama za maisha.

“Kwa kiwango kikubwa, mfumuko wa bei haujatokana na tatizo la kisera wala uamuzi wa kiutawala au uzembe, bali majanga ya dunia. Yanapotokea majanga haya hatutakiwi kunyoosheana vidole, ila kumwomba Mwenyezi Mungu kuyaondoa,” alisema.

Alisema Tanzania inaagiza bidhaa nyingi, hasa za viwandani, kutoka nje ambako gharama za uzalishaji zimeongezeka kabla hazijasafirishwa kuingizwa nchini na kisha zipelekwe mikoani.

“Rais ameona tuelimishane kwanza wakati tukiangalia mwenendo wa kupanda kwa bei mpaka Juni kuangalia hatua za kikodi tunazoweza kuchukua,” alisema.

Mabwawa ya umwagiliaji

Katika kuhakikisha majanga ya dunia hayaleti athari kubwa nchini, Mwigulu alisema katika bajeti ijayo, nguvu imeelekezwa kuimarisha sekta ya kilimo kwa kujenga mabwawa ya umwagiliaji katika kila halmashauri.


Alisema Serikali imeshatoa fedha za kununua mtambo wa kuchimba visima kwa kila mkoa na kutakuwa na mtambo wa kuchimba mabwawa ya umwagiliaji kwa kila mkoa.

Mitambo hiyo inatarajiwa kukuza kipato cha wakulima na kuajiri vijana wengi watakaokuwa wanavuna zaidi ya mara moja.

“Kila mkoa pia utakuwa na mtambo wa kupima maji ili kuepuka kuchimba kisima au bwawa sehemu isiyokuwa na maji ya kutosha. Kutakuwa na skimu nyingi za umwagiliaji. Benki pia zitakuwa na dirisha maalumu la mikopo ya kilimo,” alisisitiza.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad