Kauli ya Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky kuwa nchi hiyo “itapigana hadi mwisho,” imeibua hisia ya kuwepo kwa msaada wa jeshi lake linalopambana na Russia.
Katika hotuba yake ya juzi, Zelensky alitumia maneno ya Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Winston Churchill ya mwaka 1940 kuwa, “tutapigana kwenye fukwe, hatutaacha na hatutapoteza. Tutapigana hadi mwisho baharini, angani, tutaendelea kupigania ardhi yetu, kwa gharama yoyote. Tutapigana misituni, mashambani, ufukweni, mitaani.”
Rais Zelensky pia, aliwashukuru viongozi wa Marekani na Uingereza kwa kupiga marufuku mafuta ya Russia kuingia kwenye nchi zao.
Hata hivyo, Zelensky ametumia hotuba yake ya jana kutoa wito wa majadiliano ya kukomesha vita na Russia.
Wakati Rais Zelensky akijitapa kupambana na Russia, jeshi la Ukraine limetoa video kadhaa zinazoonyesha helikopta za Russia zikidunguliwa na makombora ya kutoka ardhini hadi angani.
Baadhi ya wachambuzi wa kijeshi wanaamini kuwa kuna ushahidi kwamba silaha zilizotolewa hivi karibuni na Magharibi tayari zinatumika.
Taarifa zinaeleza kuwa kuna zaidi ya ndege na helikopta 20 za Russia zimedunguliwa na makombora ya Ukraine.
Hata hivyo, idadi hiyo ni ndogo kuliko madai ya Wizara ya Ulinzi ya Ukraine, ambayo inasema imeangusha ndege 48 za Russia na helikopta 80. Licha ya uchache huo, inaonyesha Russia imejitahidi kupambana angani.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ulinzi wa Uingereza, Ben Wallace hadi sasa Russia haijafanikiwa kuharibu ulinzi wa anga na jeshi la anga la Ukraine.
Kabla ya vita kuanza, ndege za kijeshi za Ukraine zilizidiwa angalau tatu kwa moja na zile zilizokusanywa kwenye mpaka na Russia.
Wallace alisema uwezo wa Ukraine wa kuweka baadhi ya ulinzi wa angani tayari ulikuwa unalazimisha ndege za Russia kuruka usiku ili kuepuka kugunduliwa na makombora ya ulinzi wa anga yanayorushwa kwa mabega yakijulikana kama Manpads.
Hizo ni miongoni mwa silaha zilizotolewa na mataifa ya Magharibi kwa Ukraine. Taarifa zinaeleza kuwa, makombora aina ya Stinger yaliyotengenezwa na Marekani yanayoshambulia kutoka ardhini hadi angani yanazipa wakati mgumu ndege za Russia.
Waziri Wallace aliwaambia waandishi wa habari hivi karibuni kuwa nchi za magharibi sasa zimewasilisha maelfu ya silaha za kupambana na tanki na Stingers zaidi ya elfu.
Shirika la Habari la CNN la Marekani, limemnukuu ofisa wa ulinzi wa Marekani akisema nchi hiyo iliweka jumla ya silaha za vifaru 17,000 na Stingers 2,000, zilizotumwa na washirika wake na Nato. Uingereza na Marekani zilikuwa zimetoa silaha kwa Ukraine kabla ya uvamizi huo kuanza Februari 24 na Uingereza kuwasilisha makombora 2,000 mepesi ya kukinga vifaru.
Alipoulizwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), kama silaha hizo zimeanza kutumika, Waziri Wallace alijibu, “tuna ushahidi usio na kifani wa kuthibitisha hilo.”
Inakadiriwa kwa jumla, kuna mataifa 14 yaliyosambaza silaha Ukraine, zikiwamo Sweden na Finland ambazo zote zina historia ndefu ya kutoegemea upande wowote na si wanachama wa Nato, lakini zimetuma maelfu ya silaha za kupambana na vifaru nchini Ukraine.
Ujerumani imesambaza silaha 1,000 za vifaru na makombora 500 ya Stinger.
Mataifa ya Baltic pia, yamewasilisha maelfu ya silaha ikiwa ni pamoja na makombora ya Stingers na Javelin, mojawapo ya silaha bora zaidi za kupambana na vifaru duniani kwa umbali wa kilomita 2.5 (maili 1.5). Hivi karibuni kumekuwa na taarifa za usafirishaji wa silaha, zikiwamo bunduki za kivita, migodi ya kukinga vifaru na mamia ya tani za risasi, pamoja na silaha za mwili na helmeti, na vifaa vya matibabu. Silaha zote hizo ndizo zinaipa jeuri Ukraine, ambayo sasa inadai imefanikiwa kuharibu vifaru kadhaa vya Urusi T-72.
Silaha zinapitaje?
Uingereza inasema inasaidia kuwasilisha silaha hizo. Japo maofisa wa Magharibi hawaelezi wazi jinsi vifaa vinavyopatikana, lakini kwa kadri Russia inavyotekeleza operesheni zake mashariki mwa Ukraine, mtiririko wa watu na vifaa kutoka Magharibi mwa nchi hiyo umeendelea kupitia mataifa jirani ya Ulaya. Mataifa ya Estonia, Sweden na Denmark yamekiri kuwa silaha zao zilifuatiliwa na kufanikiwa kufika Ukraine wiki za hivi karibuni.