UKIACHA stori za uvamizi wa Urusi kwa Ukraine, nyingine iliyoshtua hivi karibuni na kuibua mjadala mkali ni ile ya King Kiba; mfalme wa Bongo Fleva na C.E.O wa Lebo ya Kings Music na mkewe, Amina.
Kwa mujibu wa vyombo vingi vya habari nchini Kenya, Amina alimtuhumu Kiba kuacha ndoa yao.
Ilisemekana kwamba, Amina alitaja ukafiri, matusi na kukatishwa tamaa kutoka kwa wakwe kuwa miongoni mwa mambo yaliyomfanya kuafikiana kuhusu kuvunjwa kwa muungano huo.
Amina alisema hii ilianza miezi sita tu baada ya harusi.
Ilidaiwa kwamba, mnamo Februari 10, mwaka huu Mahakama ya Kadhi huko Mombasa ilimpa Kiba siku 15 ambapo kesi hiyo itaendelea bila kuwepo kwake.
“Iwapo utashindwa kufika ndani ya muda uliotajwa hapo juu, mlalamikaji anaweza kuendelea na shauri na hukumu iliyotolewa wakati haupo,” ilisomeka amri ya Mahakama ya Kadhi.
Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, Januari 8, mwaka jana, Amina alikwenda Mahakama ya Kadhi akitaka kukatisha ndoa yake na Kiba.
Ilidaiwa kwamba, Amina alisema hakuwa akitengenezewa mazingira salama na yenye utulivu katika nyumba ya ndoa yao jijini Dar.
“Mlalamikiwa (Kiba) amefanya mzaha kwa ndoa yao kwa kujihusisha bila heshima katika maonyesho ya hadharani ya uasherati na wanawake mbalimbali kwa kutojali kabisa hisia za mwombaji,” ilisomeka karatasi ya amri hiyo.
Amina alidaiwa kuwa alisema baada ya kuzaliwa kwa mtoto wao wa kwanza Februari 19, 2019, Kiba alimwacha bila chakula au mahitaji ya msingi nyumbani kwao na alikuwa akinyonyesha wakati huo.
“Katika hayo yaliyotangulia, ni wazi kuwa mlalamikiwa (Kiba) amekuwa akifanya mambo ambayo hayakutarajiwa kwa mtu aliyeolewa na kutojali kabisa hisia za waombaji, hivyo kusababisha maumivu, uchungu, mateso ya kiakili, huzuni na mateso ya kisaikolojia,” ilisomeka karatasi ya mahakama.
Amina alikaririwa akisema; “Ndoa imevunjika kwa kiasi kikubwa na hakuna nafasi ya kuokolewa.”
Ilidaiwa kwamba Amina alitaka ndoa hiyo ivunjwe na kudai malipo ya shilingi 200,000 za Kenya sawa shilingi milioni 4 za Kitanzania kila mwezi kwa ajili yake na watoto.
Hata hivyo, habari njema na shangwe kama lote ni baada ya Kiba kutinga mjini Mombasa nchini Kenya na kuungana na familia yake kwa mara nyingine, jambo linalotafsiriwa ni hatua nzuri ya kumaliza tofauti zao.
Hii ni baada ya kusambaa kwa video mpya ya Kiba kwenye mitandao ya Kenya ikimuonesha akicheza na wanawe wawili wa kiume aliojaaliwa na Amina, Keyaan na Kamran.
Kwenye video hiyo; Kina anasikika akimuita mwanawe mdogo Kamran na kumtaka aweke pozi kwa ajili ya picha huku ikisikika sauti ya mwanamke ambaye inaaminika ni ya mama yao.
Baadhi ya mashabiki wameonesha kufurahishwa na kitendo hicho wakiamini sasa mambo ni mazuri kwenye ndoa yake kwani hicho ni kiashirio tosha kuwa ameyamaliza na mkewe, Amina.
Kiba na Amina walifunga ndoa mnamo Aprili 19, 2018 huko Mombasa nchini Kenya ambapo wamekuwa wakipitia vipindi tofauti kama zilivyo ndoa nyingi kwa sasa.
STORI; SIFAEL PAUL, DAR