Muvi iliyompa Will Smith tuzo ya Oscar ni King Richard. Hii muvi inaelezea maisha ya wacheza tennis wawili wakubwa, Venus William na ndugu yake, Serena.
Ninaipenda sana muvi hii, tena sana kwa kuwa inaleta tumaini hasa pale mtu unayepambania ndoto zako siku zote. Kwenye kupambania ndoto hizo, kuna vikwazo vyote ila ni lazima uvivuke.
Tusiwaone watu wamefanikiwa, wanaendesha magari ya mamilioni ya pesa, wana majumba ya kifahari, makampuni makubwa, jua wamepitia njia nyingi sana, na inawezekana njia walizopitia wao wewe ungeshindwa.
Kwenye maisha haya, hakuna tajiri atakayekwambia stori halisi ya maisha yake, wengi watakwambia mambo machache ambayo kwa akili yako tu utahisi ni rahisi, ila hawatokwambia yale magumu waliyopitia.
Leo tunasema Bakhresa alikuwa fundi viatu. Bro! Ufundi wa Bakhresa haukuwa huo unaoujua wewe. Baba yake alikuwa na pesa, miaka hiyo walikuwa na biashara fulani waliyokuwa wakiifanya (Nakumbuka kama ya kuoka mikate)
Sasa alichoamua mwamba ni kuanza kununua ngozi nje na kutengeneza viatu. Hapo unauona utofauti. Ngozi alizokuwa akizinunua si za elfu kumi, unazungumzia mamilioni ya pesa.
Aliifanya kazi hiyo kwa miaka, ikamtoa na kuwa bilionea mkubwa mpaka sasa hivi. Liweke hili akilini, unaposikia Bakhresa alikuwa mshona viatu, usimfananishe na yule mshona viatu anayefanya kazi hiyo mtaani kwenu. Huyu alikuwa tofauti kwa kuwa tayari aliwekeza mamilioni ya hela, na viatu alivyokuwa akitengeneza vilikuwa vya pesa ndefu.
Ukiachana na huyo, kuna mtu anaitwa Mohammed Dewji. Leo kuna watu wanamcheka kwa kusema utajiri wake ni wa kurithishwa. Haya ni maneno ya watu wenye wivu, masikini na wenye chuki na utajiri wa watu. Liepuke sana hili, linakufukuzia baraka ya mafanikio.
Tumpongeze Mo, unajua kwa nini? Ni wazazi wangapi waliamua kuwapa utajiri watoto wao, biashara kubwa, makampuni makubwa na bado wakafeli? Mzee Dewji alimpa mwanaye elimu ya biashara, baada ya hapo akampa dola milioni 40 ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 80 afanye biashara, kwa sababu alikuwa na akili ya biashara, leo ana dola bilioni 1 pointi kadhaa.
Hebu fikiria, kutoka dola milioni 40 mpaka dola bilioni moja, ni pesa ndefu sana. Sisi watoto wa Kiswahili, wazazi wetu wanapopata pesa, hatutaki kusoma tena, hatutaki kufanya biashara kwa kuwa tunahisi wazazi wetu wataishi milele.
Mzazi anatamani usimamie biashara zake, ili zikue, ni lazima uende darasani, ila hutaki kwenda, matokeo yake, ukipewa leo, baada ya miaka miwili, zimekufa. Tumpongeze kwanza mzee Dewji kwa kuwekeza kupitia mwanaye, wazazi wengi wanashindwa kufanya hivi, wengi hawawaamini watoto wao kutokana na matendo yao.
Nikirudi kwenye muvi, mzee Richard alipambania ndoto za watoto wake, wafanikiwe, wawe wacheza tennis wakubwa duniani. Aliwapa ushindi wakiwa watoto wadogo, na mwisho wa siku, wakaamini, wakapambana na kufanikiwa kupata kile walichoambiwa na baba yao tangu wakiwa wadogo.
Kupigwa kofi kwa Chris Rock, alistahili. Siku ya kwanza kwa Leonardo DiCaprio kushinda tuzo za Oscar maishani mwake kupitia muvi ya Revenant, alipokea tuzo halafu akaishika kwa staili ya kuwaonyesha dole la kati wote waliokuwa wakimdhihaki, wakimsema vibaya, hilo likazungumziwa kila kona duniani. Sasa jana naye Will Smith akafanya tukio ambalo limekuwa gumzo duniani.
Wajuzi wa Mambo wanadai kwa tukio hilo movie hiyo imepata kiki kubwa sana kiasi kwamba ndani ya hii wiki inatarajiwa mauzo yatapanda kuliko kawaida
Jamii Forums