Korea Kaskazini, Syria, Balarus zaiunga mkono Urusi UN
WAKATI Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa likiketi na kupiga kura kuikemea Urusi na kutaka majeshi yake yanayofanya operesheni nchini Ukraine kuondoka mara moja, mataifa matano yamepinga uamuzi huo.
Belarus, Syria, Korea ya Kaskazini, Eritrea na Urusi yenyewe zilipiga kura ya hapana wakati mataifa 141 yakipiga kura ya ndio.
India, Afrika Kusini, Irag, Iran, Cuba na Kazakhstan ni miongoni mwa mataifa 35 wanachama wa baraza hilo ambayo yalijizuia kupiga kura yoyote.
Matokeo ya kura ya Jumatano yanafuatia kura iliyopigwa Ijumaa iliyopita na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo Urusi ilitumia kura yake ya turufu kuzuia rasimu ya azimio la kulaani uvamizi huo.
Huku wajumbe wengine wote wa Baraza la Usalama wakiwa wamepiga kura ya kuunga mkono au kutopiga kura, rasimu ya azimio hilo iliruhusiwa kuwasilishwa katika kikao cha kwanza cha dharura cha Baraza Kuu tangu mwaka 1997.