Kumekucha Fedha za UVIKO-19, Mkaguzi Mkuu Afunguka




KUMEKUCHA! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kutangaza kuwa ameanza kufanya ukaguzi maalumu wa matumizi ya fedha za UVIKO-19 zilizopelekwa kwenye halmashauri nchini.

Vilevile, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Katanga, amekubali kushughulikia ombi la Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) kupatiwa watumishi 104 ili kuondokana na kuchelewa kwa ukaguzi kwenye maeneo mbalimbali nchini.

CAG, Charles Kichere, alibainisha kuanza kwa ukaguzi huo maalumu jana wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi hiyo kilichofanyika jijini hapa.

“Tunampongeza Mheshimiwa Rais Samia kwa namna anavyokabiliana na janga la UVIKO-19. Ninampongeza Rais kwa namna alivyotoa maelekezo ya matumizi ya fedha za kukabiliana na UVIKO-19, hususan afya, elimu, maji na hatua anazochukua za kudhibiti matumizi ya fedha hizo,”alisema.

Alibainisha kuwa katika kuunga mkono jitihada hizo, ofisi yake imeanza kutekeleza jukumu lake la kikatiba kwa kuanza ukaguzi kwenye halmashauri zilizopata fedha hizo.

“Mheshimiwa mgeni rasmi (Katibu Mkuu Kiongozi) nikuhakikishie kwamba tutafanya ukaguzi wa fedha hizo zote za UVIKO-19 zilizoletwa na kila senti ya fedha hizo itakaguliwa na taarifa itatolewa, ili kuhakikisha fedha hizo zimetumika kulingana na maelekezo, taratibu, sheria na miongozo ya matumizi ya fedha za umma,” alisema.

Akifungua kikao hicho, Balozi Katanga alikubali ombi la ofisi hiyo kupatiwa watumishi 104 ili kukabiliana na upungufu uliopo unaosababisha baadhi ya shughuli za ukaguzi kuchelewa.

Alisema lengo kubwa ni kuiwezesha ofisi hiyo kufanya kazi kwa weledi huku akiwaasa kujiepusha na vitendo vya utovu wa nidhamu, ikiwamo kupokea rushwa wakati wanatekeleza majukumu yao.


“Ni dhamira ya serikali kuhakikisha fedha zinazopelekwa kwenye miradi ya maendeleo zinatumika vizuri na thamani ya fedha inapatikana,” alisema.

Balozi Katanga alisema kuwa katika kupunguza hoja za ukaguzi kwenye wizara na taasisi za umma, ni vyema ofisi yake na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali washirikiane ili kuhakikisha kunakuwa na uwazi na uwajibikaji kwenye mapato na matumizi ya rasilimali nchini.

“Ofisi hii inapaswa kufanya kazi kwa uhuru bila kuingiliwa na mtu yeyote. Niwapongeze sana watendaji kwa kutoa ripoti na kutekeleza majukumu ya ukaguzi maalum ambao huombwa na viongozi au taasisi,” alisema.

Awali, Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Ofisi hiyo, Godfrey Mgomi, alisema lengo ni kujadili na kujibu hoja za watumishi kupitia mpango mkakati wa ofisi hiyo, kupitia maoteo ya bajeti na kupata tathmini ya utekelezaji wa bajeti inayoisha 2021/22.

Mwaka jana, Tanzania ilipatiwa mkopo wa dharura wa Sh. trilioni 1.29 na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa ajili ya kukabiliana na athari za ugonjwa wa UVIKO-19. Kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 230 zilipelekwa Tanzania Zanzibar.

Baada ya kuripotiwa kuwapo hofu ya 'upigaji' wa fedha hizo katika baadhi ya halmashauri, serikali iliagiza kufanyike ukaguzi maalumu kuhusu matumizi ya fedha hizo, huku Rais Samia Suluhu Hassan akionya kuwa yeyote atakayebainika kufuja fedha hizo 'ataijua sura yake halisi'.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad