MKUU wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba, amewataka wadau wa biashara nchini kuandaa mwongozo utakaowezesha madalali na mawakala kurasimishwa ili walipe kodi itakayosaidia kazi hiyo kuchangia pato la taifa.
Alisema serikali inapoteza fedha nyingi kwenye sekta hizo kwa sababu hakuna mfumo rasmi wa kuwatoza kodi licha ya watu hao kukusanya fedha nyingi kupitia shughuli wanazozifanya.
Mgumba aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akifunga mafunzo ya Sheria na Leseni kwa maofisa biashara wa halmashauri kutoka mikoa mitatu ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambayo yaliandaliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).
Mafunzo hayo yaliwashirikisha maofisa biashara zaidi ya 50 kutoka katika halmashauri za mikoa ya Mbeya, Songwe na Rukwa na kufanyikia jijini Mbeya kwa muda wa wiki moja.
Mgumba alisema ni wakati wa wataalamu hao wa biashara kuwa wabunifu kwa kuwa na jicho la kuibua vyanzo vingine vipya vya mapato ili kuiongezea serikali mapato yatakayoisaidia kutekeleza miradi ya maendeleo.
“Niwaombe BRELA na maofisa biashara mkakae muone ni kwa namna gani mnaweza kuwarasimisha madalali kwa sababu katika eneo hili serikali imekuwa ikipoteza mapato mengi sana, mwenye nyumba hamfahamu mpangaji wake, madalali wamekuwa watu wa katikati na wanapata fedha nzuri sasa,” alisema Mgumba.
Alisema endapo kundi hilo litatambuliwa na kuwekewa miongozo na wakapatiwa leseni, serikali itapata fedha na wao wataendelea kupata fedha kwa ajili ya kuendeleza maisha yao.
Hata hivyo, mkuu huyo wa mkoa aliwataka maofisa biashara kuwa daraja kati ya wafanyabiashara na serikali na kutokuwa kikwazo cha biashara za watu kukua na wala wawekezaji kuogopa kuwekeza kwenye halmashauri zao.
“Ukiona katika eneo lako biashara zinafungwa na wewe upo ni lazima ujitathmini kama unatosha, nadhani hicho ndiyo kipimo cha utendaji kazi wako, pia hapo nisisitize ni lazima mtoe elimu kwa wafanyabiashara badala ya kufikiria kuwafungia,” alisema Mgumba.
Ofisa Uhusiano wa BRELA, Rhoida Andusamile, alisema mafunzo hayo yaliyowakutanisha maofisa biashara kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini yamelenga kuongeza ufanisi katika masuala ya usimamizi wa biashara.
Alisema pia kupitia mafunzo hayo maofisa biashara na BRELA wamekumbushwa mipaka yao ya kazi ili kutoingiliana katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.