JANA Machi 14, 2022 Rais Samia Suluhu Hassan alimteua Nehemia Mchechu kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), pamoja na viongozi wengine.
Mchechu amerejea kwenye nafasi aliyokuwa akiishikilia tangu mwaka 2010 hadi 2018 alipotenguliwa, akiingia kwenye nafasi hiyo baada ya kuiongoza Benki ya Biashara ya Afrika ‘Commercial Bank of Africa’.
Akiwa mkurugenzi wa benki hiyo, Mchechu alichanua, utendaji kazi wake ukang’aa kutokana na mafaniko makubwa aliyoipatia benki hiyo; sifa ambayo huenda ndiyo iliyompatia ulaji NHC.
Mwaka 2017, nafasi ya Mchechu ilianza kuwa ya moto; tuhuma zikawa nyingi akitajwa kujilipa mshahara na marupurupu makubwa na tuhuma za kuwa na mgongano wa kimaslahi kwa madai kuwa alikuwa anamiliki kampuni ya ujenzi aliyokuwa akiitumia kupiga ‘dili’ za ujenzi.
Desemba 2017, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alimsimamisha kazi Mchechu kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili, ingawa kwenye barua yake hakuzitaja.
Kabla ya kusimamishwa kazi, habari za chini ya kapeti zilidai kuwa, hakuwa na maelewano mazuri na bosi wake wa kipindi hicho, Lukuvi na kwamba wizarani kulikuwa na ‘genge’ la watu waliokuwa wanamsagia kunguni ili aondolewe kwenye nafasi yake.
Baada ya kusimamishwa kazi, Mchechu alikaa benchi kusikiliza ‘kifuatacho.’
Presha kwenye mitandao ya kijamii na kwenye baadhi ya vyombo vya habari ilikuwa kubwa kwamba Mchechu anatakiwa kushtakiwa lakini yote kwa yote yanatajwa kuwa yalitokana na msukumo wa kutaka Mchechu aondolewe madarakani.
Juni 2018, hatimaye uteuzi wa Mchechu ulitenguliwa rasmi.
Hata hivyo, baada ya Lukuvi kung’olewa wizarani ambaye awali aliwahi kuelezwa na Hayati John Pombe Magufuli kwamba aende akatengeneze mwelekeo mpya na ‘hasimu’ ili tija iwepo, mambo yamemkalia vizuri Mchechu.
Leo (Jumanne), Mchechu amekula kiapo cha kurejea kulitumikia tena Shirika la Nyumba la NHC ambalo wengi wanasema enzi za uongozi wake lilikuwa likifanya vizuri.
Kurejea kwake kazini ni uthibitisho tosha kuwa vyombo vya usalama vimejiridhisha kuwa hakuwa ‘mpigaji’.
Mtihani mkubwa kwa Mchechu hivi sasa ni kuchapa kazi ili NHC isonge mbele kwa kasi; atamwangusha aliyemteua na itakuwa changamoto kubwa kwake?
Richard Manyota