MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Chadema Bara, Tundu Lissu, amesema chama hicho hakiko tayari kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), kwa kuwa sio kipaumbele chake. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Lissu ametoa kauli hiyo jana Jumatano,tarehe 9 Machi, 2022 kwenye mjadala uliofanyika katika mtandao wa ClubHouse, juu ya hatua ya Mwenyekiti wa Chadema Tanzania, Freeman Mbowe, kufanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya kutoka gerezani.
Ni baada ya kuulizwa iwapo Chadema kiko tayari kujiunga na SUK, kama ilivyotokea Visiwani Zanzibar, baada ya Chama cha ACT-Wazalendo, kujiunga kwenye Serikali hiyo.
“Our interest (matamanio) ni kuubadilisha mfumo wa Power (utawala), kitakacho determine (amua) msimamo wetu ni namna gani tunabadili power structure (muundo wa utawala). Ndiyo maana tunazungumza katiba, hatutaki kupigiwa saluti, tunataka kubadilisha power structure,” amesema Lissu.
Makamu Mwenyekiti huyo wa Chadema amedai, SUK sio suluhisho la utawala bora kwani, licha ya upinzani kushirikishwa bado Rais anayekuwepo madarakani ana mamlaka na ni mwenye maamuzi ya mwisho.
“Jinsi ambavyo SUK inavyoweza kuwa hatari kabisa, mnaingizwa kwenye SUK mnapewa uwaziri au mawaziri watatu watano. Wote wanateuliwa na Rais halafu katika uamuzi sababu katiba inampa mamlaka yote, mnaingizwa kwenye Serikali halafu anayafanya maamuzi yote aliyofanya jana,” amesema Lissu.
Lissu amesema “maana yake mnaingizwa kwenye Serikali, halafu maamuzi yanaendelea kuwa ya ovyo. Lakini this time inakuwa ya kwenu sababu mko ndani. Wanakushirikisha katika dhambi zao, wanakutumia kama toilet paper kuwasafisha.”
Hata hivyo, Lissu amesema SUK inayohitajika ni ile ambayo pande zote mbili zinakuwa na mamlaka sawa, katika kufanya maamuzi.
“SUK inayohitaji ni ile tunaingia serikalini nafasi zote za uteuzi ambazo Rais alikuwa anafanya uteuzi tutazigawana, tutafanya uteuzi pamoja. Hutafanya maamuzi yoyote uliyokuwa unafayanya zamani bila kukubaliana na sisi,” amesema Lissu na kuongeza:
“You share power not position (unashiriki nguvu sio nafasi). Kuna utofauti wa ku-share nafasi na ku-share power, sasa SUK mnayo-share position mtapewa vyeo kama watu wanataka madaraka. Sisi hatuna masilahi ya kupata vyeo, mishara na majina yanayoendana na vyeo.”
Msimamo huo wa Lissu umekuja siku chache baada ya Rais Samia kuzungumza na Mbowe, tarehe 4 Machi 2022, ambapo walikubalina kufanya siasa za kistaarabu na kiungwana.
Pia, walikubaliana kushirikiana katika kuijenga Tanzania kwa kuaminiana na kuheshimiana kwenye misingi ya haki.
Mbowe alizungumza na Rais Samia, baada ya kufutiwa mashtaka ya ugaidi yaliyokuwa yanamkabili na walinzi wake, Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdilah Ling’wenya, katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, jijini Dar es Salaam.
Mashtaka hayo yaliyokuwa kwenye kesi ya uhujumu uchumi namba 16/2021, yalifutwa na mahakama hiyo mbele ya Jaji Joachim Tiganga, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Sylvester Mwakitalu, kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea nayo.
Mbowe alisota rumande kuanzia mwishoni mwa Julai 2021 hadi mwanzoni mwa Machi 2022, alipoachwa huru.