ZAIDI ya wananchi 10,000 wa Serbia, wameingia mitaani na kuandamana katika Jiji la Belgrade kuelekea katika ubalozi wa Urusi nchini humo, kama njia ya kuonesha kumuunga mkono Rais Vladimir Putin katika uvamizi wake nchini Ukraine.
Maandamano hayo ndiyo ya kwanza na makubwa kuiunga mkono Urusi, yamefanyika hapo jana, Ijumaa Machi 4, 2022 ambapo waandamanaji walikuwa wamebeba picha za Putin, bendera za Urusi na mabango yenye ujumbe mbalimbali kuiunga mkono Urusi.
Hoja kubwa inayotolewa na waandamanaji hao, ni kwamba Ukraine haipaswi kuruhusiwa kujiunga na NATO kwa sababu umoja huo wa kujihami, umewahi kuishambulia Serbia katika mapigano ya Kosovo mwaka 1990 na kusababisha madhara makubwa ambayo hayajasahaulika hadi leo.
Baadhi ya wananchi wa Serbia wanaiona Nato kama adui yao na hivyo wameamua kusimama na Urusi ambayo kipindi Nato inaishambulia Serbia, ilisimama kuwatetea na kuipinga Nato hadharani mpaka mwisho.