Sehemu ya mahojiano kati ya Watson Mwahomange (27) Shahidi namba saba upande wa utetezi na Wakili wa Jamhuri.
WAKILI: Wewe na Sabaya mlikua na mahusiano gani?
WATSON: Alipokua Mkuu wa wilaya Hai, mimi nilikua msaidizi wake upande wa picha.
WAKILI: Wewe ni mtumishi wa umma?
WATSON: Hapana.
WAKILI: Uliwezaje kuwa msaidizi wa DC bila kupitia taratibu za utumishi?
WATSON: Aliniajiri yeye binafsi, sio serikali.
WAKILI: ieleze mahakama hii uhusiano wenu na Sabaya ulianza lini?
WATSON: Mimi ni mpiga picha. Mwaka 2019 Sabaya alinipa kazi ya kumpiga picha akiwa ibadani Kanisa la KKKT, Azimio kwenye ibada iliyoongozwa na Askofu Masangwa. Baada ya hapo akaniambia atanipa ajira niwe mpiga picha wake.
WAKILI: Alikupa mkataba wa ajira?
WATSON: Hapana, lakini alikua ananilipa mshahara tuliokubaliana kila mwezi.
WAKILI: Mliishi pamoja?
WATSON: Niliishi na wasaidizi wengine wa Sabaya watano, jumla tukawa 6.
WAKILI: Kwa muda uliofanya kazi na Sabaya umewahi kushuhudia akifanya matukio ya kihalifu?
WATSON: Mengi tu mheshimiwa.
WAKILI: Unafahamu kesi inayowakabili?
WATSON: Ndio.
WAKILI: Itaje.
WATSON: Kuunda genge la uhalifu na kutakatisha fedha kiasi cha TZS 90 milioni.
WAKILI: Tukio hilo mlifanya kwa nani?
WATSON: Kwa Francis Mrosso.
WAKILI: Ulikuwepo?
WATSON: Ndio, lakini sikushiriki. Hata CCTV zinanionesha nikiwa pembeni.
WAKILI: Kwanini hukuripoti?
WATSON: Nilihofia usalama wangu. Sabaya ni mtu hatari, angeweza kunidhuru.
WAKILI: Kwanini uliendelea kufanya kazi na mtu hatari?
WATSON: Kwa sababu kuachana nae ilikua hatari zaidi.
WAKILI: Kipi kinachokufanya useme Sabaya ni mtu hatari?
WATSON: Kulingana na matukio yake aliyokua akifanya. Hata sisi wasaidizi wake tuliishi kama mateka. Mimi aliwahi kunipiga kwa kushirikiana na polisi hadi kuzirai.
WAKILI: Uliripoti polisi?
WATSON: Wale alioshirikiana nao kunipiga ama wengine? (mahakama kicheko).!
WATSON: Mheshimiwa Hakimu naomba niongezewe ulinzi gerezani maana Sabaya anaweza kuniundia genge la kunidhuru.
Hakimu Mkazi Mwandamizi Patricia Kisinda anasema Mahakama itapima hoja za Watson na kuona kama kuna haja ya kuongezewa ulinzi gerezani ama lah.!