Ndani ya Jiji la Dar es Salaam kuna mnyukano. Ni baina ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na mfanyabiashara Ghalib Said Mohammed (GSM). Wanagombea ardhi.
Makonda analalamika kuwa GSM anataka kumdhulumu mali yake. Wakili wa GSM, Alex Mgongolwa akatoa ushahidi wa umiliki wa ardhi yenye mgogoro. Kwamba ni mali halali ya mteja wake.
Nani mmiliki? Hilo jawabu litajulikana mbele ya sheria. Msingi wa makala hii ni kumtazama Makonda anayelalamika kuwa anadhulumiwa na mfanyabiashara aliyemwita tapeli. Hana nguvu!
Ikikupendeza, rudi nyuma miaka mitatu tu. Je, ungedhani yule Makonda, mkuu wa mkoa, angekuwa huyu anayesema yupo tayari kupigwa risasi lakini si kushuhudia mali yake ikichukuliwa?
Yule Makonda tishio, mpaka Serikali ya Marekani ikatoa taarifa ya kumpiga marufuku kukanyaga kwenye taifa hilo, kwa sababu waliyoitaja kwamba ni kudhulumu haki ya watu wengine kuishi, ndio huyu asiye na nguvu zozote?
Makonda yule aliyevamia kituo cha Clouds TV na hakufanywa chochote. Aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alipotaka kusimama kidete haki itendeke, akajikuta yeye ndiye anafukuzwa kazi. Ndiye huyu anayelalamika polisi wanatumiwa kumdhulumu mali yake?
Yule Makonda aliyeamuru mfanyabiashara, Yusuf Manji na pesa zake akae ndani na akakaa. Aliyemlaza mahabusu Askofu Josephat Gwajima. Ongeza wafanyabiashara wengine wengi na wasanii. Huyu kawa mlalamikaji.
Makonda aliyeamuru Ridhiwani Kikwete, mtoto wa Rais wa Nne, Jakaya Kikwete, akamatwe na ahojiwe. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alikamatwa barabarani kama jambazi ili akahojiwe kuhusu tuhuma ya kuhusika na biashara ya dawa za kulevya. Ni kwa amri ya Makonda.
Wapo watu hoja yao ni uwezo wa Makonda kumiliki mali za mabilioni. Na kulilia kabisa. Kwamba kwa mshahara wake, hiyo mali ya thamani ya mabilioni angepataje?
Mimi sipo huko, nauliza; Makonda angeendelea kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, halafu nchi ingekuwa chini ya hayati Dk John Magufuli, GSM wangethubutu kugombea naye ardhi?
Unamzunguzia Makonda aliyekuwa anawaita maofisa waaandamizi wa Wizara ya Ardhi na kuwaweka ndani. Hao, wangewezaje kuthubutu kutamka mali ya Makonda bali GSM? Hapo ndio kwenye shule.
Ruhusa kuelimika
Matokeo ya sasa ya Makonda, kutoka yule ambaye alikuwa hagusiki, akitembea na ulinzi mkubwa, ni shule ambayo kila kiongozi, hasa kijana, anapaswa kutunza akilini.
Uongozi wa kisiasa hupaswi kuuendea kwa pupa. Huja na kuondoka. Ndiyo maana kuna nyakati Makonda yupo mtaani analalamika polisi hawatendi haki. Alipokuwa mkuu wa mkoa, aliwaamrisha atakavyo na wengine aliwalaza mahabusu.
Mambo matatu zingatia kabla hujaanza siasa. Mosi zina tabia ya kujaza upepo, inawezekana ukawa huna uwezo lakini ukawa tishio kwelikweli. Siasa zinaweza kukufanya ujione unakaribiana na Mungu kwa ukubwa. Siasa zinaweza kukupa sifa bora ambazo hustahili, inategemea na jinsi ambavyo upepo umeamua. Kama upepo unakupuliza kwa nguvu, unaweza kuwafanya watu wakuone kwamba hajawahi kutokea mwanasiasa mahiri duniani kama wewe.
Jambo la pili la kuzingatia unapoingia kwenye siasa ni kutambua kuwa siasa huwa na muda maalumu, yaani zina expire date. Unaweza kuwa mwanasiasa tishio mpaka taifa likawa haliwezi kuzungumza siasa bila kukutaja lakini mwisho ukifika utasahaulika kabisa. Usiingie kwenye siasa ukiamini kuwa utakuwa mkubwa kuliko wote kisha utadumu mpaka kifo kitakapokuondoa duniani, utajidanganya. Siasa usiziendee kwa miguu yote miwili, jiwekee akiba ya kuishi pembeni nje ya siasa.
Unaweza kuingia kwenye siasa lakini ukiwa umepishana na upepo, hata ufanye matukio gani utaonekana wa kawaida tu. Wenye upepo wakigusa tu hao wanang’ara, wewe unajiuliza mbona unafanya kazi kubwa na haipewi uzito unaostahili?
Jambo la tatu ni kuwa siasa usiitolee machozi. Ukiadhiriwa kwenye ulingo wa kisiasa fahamu kuwa ndiyo tabia yake. Wenye PhD wengi tu wameshawekwa benchi na wenye elimu ya msingi tu.
Usiumie sana kutochaguliwa, ukahisi kuwa labda hukujenga hoja zenye kueleweka au ulipungukiwa uwezo wa ushawishi. Elewa kuwa wanaosikiliza hoja ni watu na huchagua cha kusikiliza au wanaweza kusikiliza lakini akachagua cha kutunza kichwani. Kuelewa ni utashi.
Na kwa sababu wanaosikiliza kwa utashi wao huamua nani wayapokee maneno yake, ni hapo mtu mwenye kuzungumza pumba anaweza kupigiwa makofi na kuchaguliwa, wewe na pointi zako zote ukakataliwa. Hilo lisikuumize, wanaochagua wana utashi wao.
Ndiyo maana nimesema kuwa usiende kwenye siasa kwa kuingiza miguu yote miwili. Pima upepo kwanza, mguu mmoja utakaouacha nje, utakusaidia kukukwamua upepo wa kisiasa utakapokukataa.
Katika siasa muhimu zaidi chukua hii; Tumia mguu mmoja kupima kwanza kina cha maji baharini, ukishajiridhisha ndiyo ujiachie majini.
Wakati ukionesha umahiri wako wa kuogelea, kumbuka mahali ambapo ulihifadhi nguo zako ufukweni maana baada ya kuogolea utatakiwa kuvaa nguo zikutunzie heshima nje ya bahari.