Kaimu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), Consolata Mushi
KAMUSI Kuu ya Kiswahili, imeboreshwa kwa mara ya tatu, kwa kuongezewa maneno mapya 150, yakiwemo ya kiutamaduni, sayansi, teknolojia, siasa na ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatatu, tarehe 14 Machi 2022 na Kaimu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), Consolata Mushi, kwenye Kongamano la Pili la Idhaa za Kiswahili Duniani, linalofanyika jijini Arusha.
“Kamusi hii ina upekee kabisa, ukiangalia toleo la pili na tatu, baadhi ya upekee wa toleo la tatu la kamusi hii ni pamoja na kuongeza maneno mapya 150, ya kiutamaduni, sayansi, teknolojia, siasa na maneno yanayotokana na janga la UVIKO-19,” amesema Mushi.
Kaimu Mtendaji huyo wa BAKITA, amesema mchakato wa maboresho wa kamusi hiyo ulianza 2017, baada ya kuanza kuandikwa 2011. Ambapo ilizinduliwa bungeni jijini Dodoma Juni 2017, kisha uboreshaji wa toleo la pili ulifanyika mwaka huo.
Kamusi hiyo inazinduliwa leo na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, ambaye ndiye mgeni rasmi katika kongamano hilo linaloendelea jijini Arusha.