Mashine Mbili Zampa Kiburi Nabi




GEITA Gold kazi wanayo! Ndivyo utakavyosema baada ya Kocha Mkuu wa Yanga raia wa Tunisia, Nasreddine Nabi kufurahia kurejea uwanjani mastaa wake wawili.

Timu hizo zinatarajiwa kuvaana Jumapili hii katika mchezo wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kupigwa saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Mastaa hao waliorejea katika kikosi cha kwanza ni beki wa kati, Dickson Job aliyemaliza kifungo cha kukosa michezo mitatu na kiungo mchezeshaji fundi, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyemaliza adhabu ya kadi tatu za njano.

Fei Toto tangu kuanza kwa msimu huu, amekuwa akichezeshwa nyuma ya mfungaji tegemeo wa timu hiyo, Mkongomani, Fiston Mayele kwa ajili ya kumpigia basi za mabao, huku akifunga mwenyewe akipata nafasi.


 



Akizungumza na Spoti Xtra, Nabi alisema Job na Fei Toto wanatarajiwa kuwepo sehemu ya kikosi chake kitakachowavaa Geita Gold.

Nabi aliongeza kuwa, kurejea kwa mastaa hao kutampa wigo mpana wa kuchagua wachezaji wa kuanza katika kikosi cha kwanza kutokana na ubora wa kila mmoja anauonesha anapopata nafasi.

“Ninafurahia kuona ushindani mkubwa ukiongezeka katika timu yangu, hali inayonipa ugumu wa kupanga kikosi cha kwanza kutokana na kila mchezaji kuwepo katika kiwango bora.


“Katika mchezo ujao wa ligi dhidi ya Geita Gold ninatarajia kuwatumia wachezaji wangu wawili waliokosekana katika michezo iliyopita kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo adhabu. Job alifungiwa michezo mitatu na Fei Toto alikuwa akitumikia adhabu ya kadi tatu za njano.

“Hivyo upo uwezekano mkubwa wa kuwepo mabadiliko katika kikosi changu cha kwanza, hivyo tutaingia uwanjani tukiwa imara na fiti kwa ajili ya kuchukua pointi tatu ambacho ndiyo muhimu kwangu ili tufanikishe malengo yetu ya kubeba ubingwa wa ligi msimu huu,” alisema Nabi.

WILBERT MOLANDI, DAR

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad