MASTAA wa Simba waliokuwa mapumziko ya muda mfupi na wale waliokuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars wameitwa fasta kambini na Kocha Pablo Franco anayekuna kichwa juu ya mechi yao ijayo dhidi ya US Gendermarie ya Niger.
Simba itakuwa wenyeji wa USGN katika mechi ya mwisho ya Kundi D itakayoamua hatma ya kwenda robo fainali ama kuaga michuano, lakini ikisikilizia pia katika pambano la Asec Mimosas ya Ivory Coast na RS Berkane zilizopo kundini humo.
Mechi hiyo itakayopigwa Jumapili ijayo kuanza saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ni kama fainali kwa Simba na kocha Pablo kwa kutambua ugumu na umuhimu wake aliomba wachezaji waliopo Stars waruhusiwe kujiunga na kambi.
Bahati nzuri Kocha wa Stars, Kim Poulsen amelipokea ombi hilo na kuwaruhusu wachezaji hao ambao wote sasa wametakiwa kuungana na wenzake kuanzia leo kwa kambi ya mazoezi kwa ajili ya mchezo huo dhidi ya USGN unaosubiriwa kwa hamu.
Katika michezo mitano iliyopita, Simba imeonyesha udhaifu hasa kwenye kucheza mipira ya krosi na ile ya friikiki, kitu ambacho Pablo na wasaidizi wamepanga namna ya kutibu tatizo hilo kabla ya mchezo huo wa Jumapili.
Dakika 450 ambazo ni mechi tano, Simba ilipata kona 24, ila ilifunga bao moja tu kwa njia hiyo dhidi ya Gendarmerie Februari 20, mchezo uliomalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1, huku mfungaji akiwa ni Bernard Morrison.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha msaidizi wa Simba, Seleman Matola alisema changamoto zote zilizotokea wanaanza kuzifanyia kazi leo lengo ni kuhakikisha hawarudii makosa katika mchezo wao wa mwisho.
“Mchezo wa mwisho ni muhimu sana kuliko iliyopita hivyo makosa tumeyaona na tutayarekebisha, hatutaki tena yatokee kwa sababu tunahitaji kufikia malengo ya kuifikisha timu hatua ya robo fainali.” alisema Matola.
Wapigaji wakubwa wa mipira ya kona kwa upande wa Simba katika mashindano haya ya kimataifa ni Larry Bwalya ambaye kwenye mchezo mmoja tu dhidi ya ASEC Mimosas Uwanja wa Benjamin Mkapa alipiga jumla ya kona sita.
Mwingine ni beki Shomari Kapombe ambaye ana bao moja kwenye michuano hii alilolifunga kwa mkwaju wa penalti dhidi ya ASEC Mimosas.
Katika Kundi ‘D’ Simba inashika nafasi ya tatu na pointi saba sambamba na RS Berkane nyuma ya ASEC Mimosas yenye pointi tisa huku ushindi kwao utawahakikishia kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.
MASHABIKI 35,000 KAMA KAWAIDA
Meneja Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Ahmed Ally alisema wameruhusiwa kuingiza mashabiki 35, 000 na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) katika mchezo huo ikiwa ni idadi inayotumika siku zote japo walitamani zaidi kutokana na umuhimu wa mechi yenyewe.