Matumizi Holela ya Dawa yatajwa Kusababisha Ugonjwa wa Figo




Matumizi holela ya dawa za asili na vidonge jamii ya 'Diclofenac' ili kupunguza maumivu ya mwili yanaelezwa kuwa kisababishi kikubwa cha magonjwa ya figo nchini.

Mbali na matumizi ya dawa hizo, visababishi vingine ni pamoja na shinikizo la juu la damu, kisukari kisichodhibitiwa, ulevi kupindukia, kukosa mazoezi ya mwili na maambukizi katika njia ya mkojo.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya Figo duniani kwa mkoa wa Mwanza yaliyofanyika katika hospitali ya rufaa ya Kanda ya Bugando jijini Mwanza Daktari bingwa wa magonjwa ya figo, Dk Ladius Rudovick amesema hospitali hiyo inahudumia wastani wa wagonjwa wenye matatizo ya figo 200 kwa siku.

"Ili kuepuka kuingia gharama kubwa kutibu magonjwa ya figo ni vyema watu wakajijengea utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kubaini iwapo wanatatizo hilo ama lah, hii itasaidia iwapo mtu atakugundulika kuwa na ugonjwa kuanza matibabu kabla haujafika kwenye hatua mbaya," amesema Dk Rudovick


Pia amesema unene kupindukia unachangia kwa kiasi kikubwa ugonjwa wa shinikizo la damu ambalo ni miongoni mwa visababishi vya ugonjwa wa figo huku akitoa wito kwa jamii kufanya mazoezi na kupunguza kula vyakula vyenye mafuta ili kuepukana na unene uliopitiliza.

Mkurugenzi wa Tiba Bugando, Dk Bahati Wajanga amesema kwa kutambua umuhimu wa siku ya figo duniani hospitali hiyo inatoa huduma ya ushauri na vipimo bila malipo.

"Ni vizuri wananchi na wakazi wa Kanda ya Ziwa wakajitokeza kuchangamkia fursa hii maana matibabu ya figo ni gharama kubwa lakini wiki hii tunayatoa bila malipo," amesema Dk Wajanga


Naye Mkazi wa Igoma jijini Mwanza Ester Pastory ameishukuru hospitali hiyo kwa kutoa huduma hizo bila malipo huku akisema kufanya hivyo kutasaidia kuokoa maisha ya wananchi walioshindwa kumudu gharama za matibabu hayo.

"Niwaombe wasiishie kutoa huduma hapa mjini, wapanue zaidi na kwenda vijijini ambako kuna wananchi wengi wanaosumbuliwa na tatizo hilo na hawawezi kuja mjini kupata matibabu kwa hofu ya kushindwa kumudu gharama," amesema Ester

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad