LICHA ya kuwa yeye ndiye kinara wa mabao kwenye ligi kwa sasa akiwa sawa na Reliants Lusajo wa Namungo, mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele, amesema haitakuwa rahisi kwake kuchukua kiatu hicho.
Mayele ameweka wazi kuwa, kila mshambuliaji anataka kuwa mfungaji bora mwisho wa msimu, hali ambayo inaongeza uzito na ushindani kwenye kuwania tuzo ya mfungaji bora mwisho wa msimu.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Mayele alisema anatamani kuwa mfungaji bora mwisho wa msimu, lakini haitakuwa rahisi sana, kwa sababu kila mchezaji anahitaji tuzo hiyo, ndiyo maana hawajaachana sana kwenye idadi ya mabao ambayo wamefunga.
“Kiatu cha ufungaji bora ni kigumu sana kwa sababu kila mchezaji anayo nafasi ya kuchukua kiatu hicho. Natamani ndiyo na ninaweza kuwa mfungaji bora, ila haitakuwa rahisi sana,” alisema.
Mayele amefunga mabao 10 kwenye ligi, sawa na Lusajo, na kutoa asisti tatu kwenye mechi 17 ambazo Yanga wamecheza hadi sasa.
George Mpole anafuatia akiwa na mabao 8, wakati Said Ntibazonkiza (Yanga), Vitalis Mayanga (Polisi) na Meddie Kagere (Simba) wamefungana wakiwa na mabao 6 kila mmoja. Jeremiah Juma wa Prisons ana mabao 5, lakini timu yake ipo mkiani mwa msimamo wa ligi kuu.
Issa Liponda,
Dar es Salaam