Hakukuwa na mtu hata mmoja wa familia karibu na Dmytro Kotenko wakati alipozikwa.
Wazazi wake hawakusikia milio ya risasi kama ishara ya heshima kwenye kaburi lake. Hawakusikia hata sauti ya utepe ukifungwa kwenye msalaba wa mbao upepo ukivuma.
Wazazi wa Kotenko walikuwa umbali wa kilomita 600, huko Sumy, bila kujua mtoto wao alikuwa akizikwa siku hiyo huko Lviv.
Baadhi ya wanajeshi wa Ukraine waliofariki hawawezi kupelekwa nyumbani kwa sababu Urusi inashambulia miji yao, na familia zao haziwezi kuja kuzika makaburini kwa sababu ya hatari ya kushambuliwa na makombora.
Siku ambayo Kotenko alizikwa, kulikuwa na mtu mmoja tu aliyemfahamu makaburini- rafiki yake wa shule Vadym Yarovenko, ambaye alikuwa anafanya kazi Lviv.
"Nilitazama rafiki yangu akizikwa mbali na nyumbani kwake," Yarovenko alisema.
Dmytro Kotenko alifariki katika siku ya tatu ya uvamizi wa Urusi. Alifariki akiwa na umri wa miaka 21.