Tanga. Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Makame Mbarawa ametoa siku nne kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kutoa maelezo ya kupuuza agizo lake la kuitaka mamlaka hiyo kuwaalika vijana kutoka vyuo vya uhandisi katika Bandari ya Tanga ili kupata ujuzi kwa vitendo wakati wa mradi wa ujenzi unaoendelea bandarini hapo.
Mbarawa ametoa agizo hilo leo Jumanne Machi 8, wakati alipotembelea Bandari ya Tanga kukagua maendeleo ya ujenzi wa uongezaji wa kina cha bandari hiyo pamoja na gati la kisasa.
"Nilikuja mara ya mwisho hapa Desemba mwaka jana nikatoa maagizo vijana wetu wanaomaliza Shahada ya Uhandisi waje hapa kujifunza wakati ujenzi unaendelea ili ujuzi huu usipotee vijana wetu wakijua hatutakuwa na haja ya kuchukua makampuni kutoka nje," amesema.
Aidha, amesema atachukua hatua kali za kumhamisha Ofisa Utumishi wa mamlaka hiyo, endapo atashindwa kutoa maelezo yanayojitosheleza kwanini wamepuuza agizo hilo.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Bandari Mkoa wa Tanga, Masoud Mrisha amesema amepokea agizo la waziri na kwamba watalifanyia kazi kwa haraka.
"Mimi ni mgeni hapa Tanga wakati wakati waziri anatoa agizo hilo sikuwepo hivyo ninamuahidi Mheshimiwa Waziri nimelipokea na nitalifanyia kazi mara moja," amesema Mrisha.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima amesema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo na kwamba mradi huo utakapokamilika utasaidia kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa bandari hiyo.
,,Mheshimiwa Waziri nisema nimerishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi huu hivyo niendele kuwahimiza kwamba itakafika meimwaka huu uwe umekamilika kama wanavyotuahidi hapa,, amesema Malima.
Ujenzi wa kuongeza kina cha bandari na gati ya kisasa mkoani hapo kwa sasa umefikia asilimia 35 jambo lililosababisha Mkandarasi anayesimamia mradi huo kuomba serikali imuongezee muda mpaka mwisho wa mwezi Mei ambapo awali mradi huo ulitakiwa kukamilika mwisho wa mwezi machi mwahuu.