Mbeya City yafungwa kwa Mara ya Kwanza...



Msimu huu Mbeya City ilikuwa haijapoteza mchezo wowote nyumbani na leo Kagera Sugar wametibua rekodi na kuwa wa kwanza kupata alama tatu kwenye uwanja wa Sokoine.
Mbeya. Kwa mara ya kwanza Mbeya City imepoteza mchezo wake wa Ligi Kuu ya NBC katika uwanja wa nyumbani baada ya kukubali kulala bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar.

Pia kichapo hicho ni cha pili kwenye uwanja huo ikiwamo ya kombe la shirikisho walipolala kwa penalti 4-3 dhidi ya Afrcan Sports baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1 lakini ikiwa ni kichapo cha nne msimu huu.

Mchezo huo ambao umepigwa uwanja wa Sokoine, licha ya wachezaji kucheza sasa rafu, lakini hata presha kwa timu zote ilionekana kuwa juu hususani wenyeji, Mbeya City ambao hawakuonesha utulivu walipokuwa na umiliki wa mpira.

Hata hivyo Mbeya City hawakuonesha soka lao la ushindani na kasi lililozoeleka na kuwafanya wapinzani wao kuonekana kuutawala mchezo huku walionesha uwezo binafsi na kuwafanya kuondoka jijini Mbeya kwa kishindo kufuatia matokeo hayo.


Ilikuwa dakika ya 20, ambapo mabeki wa City walijichanganya wakidhani Hassan Mwaterema ameotea kabla ya kushuhudia wavu wao ukitikisika na mwamuzi Hance Mabena akielekeza mpira kuwekwa kati akiashiria bao kwa 'Wanankurukumbi'.

Mbeya City walijaribu kutengeneza nafasi kadhaa lakini walikosa umakini kutokana na mipira yao kutokuwa na macho ya kuliona lango na kufanya kipindi cha kaanza kumalizika wakiwa nyuma kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili City walianza kwa kasi, lakini Kagera Sugar wao wakionekana kutulia, ambapo makocha wa timu zote walifanya mabadiliko ya mbinu kwa kuwapumzisha baadhi ya nyota wao na kuingiza nguvu mpya, huku wenyeji wakiweka idadi kubwa.


Kagera Sugar waliwatoa Hamis Kiiza, Mwaterema na nafasi zao kuingia Meshack Abraham na Abdalah Seseme, huku Mbeya City wakiwatoa Frank Ikobela, Seleman Boban, Joseph Ssemuju na Richardson Ng'ondya na kuwaingiza, Paul Nonga, Shaban Kisiga, Siraji Juma na Helbet Lukindo mabadiliko ambayo hayakubadili matokeo.

Matokeo hayo yanaifanya Kagera Sugar kufikisha alama 24 na kupaa nafasi ya sita huku City wakibaki nafasi yao ya tano kwa alama 25 baada ya timu zote kucheza mechi 18.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad