Mbowe aeleza sababu zilizomkutanisha na Rais Samia

 


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Freeman Mbowe ameeleza sababu zilizomfanya akutane na Rais Samia Suluhu Hassan mara tu baada ya kutoka gerezani.


Ametumia kongamano la Baraza la wanawake Tanzania BAWACHA katika siku ya wanawake duniani kuzungumza na watanzania kuhusu mambo kuhusu kesi ya ugaidi iliyokuwa inamkabili yeye na wenzake watatu.


Amesema kesi ilipofutwa alipokea ujumbe wa Rais Samia kutaka waonane, naye hakusita kwa sababu chama chake kilikuwa kinasubiri nafasi hiyo.


“Kwa sababu mbalimbali niliridhia, kwanza binafsi na chama chetu tumetafuta nafasi hiyo bila mafanikio. Rais wa mwisho kukaa naye alikuwa Jakaya Kikwete,” amesema Mbowe na kuongeza:


“Kwa hiyo tumetafuta fursa ya kuonana viongozi kwa sababu tunajua wana-Chadema wamebeba nini vifuani mwao na tunaamini Rais ndiye mwenye funguo ya vikwazo vingi zinavyosababisha simanzi kwenye Taifa”


Mbowe ameeleza kuwa “wakati wote nilipokuwa gerezani niliomba kibali na nilikiona kibali hiki nilipopata mwaliko hivyo, zangu nilikwenda Ikulu. Nimshukuru Rais Samia kwa sababu alinipa pole, na namshukuru kwa namna mazungumzo yetu yalivyokwenda,” amesema.


“Akaniambia Mbowe nieleze shida mlizokuwa nazo, nikamwambia mama nimekuja kwako leo sio kulia shida, nimekuja kuweka misingi. Shida zitakuja baadaye lakini kwanza ili mazungumzo yoyote yajenge mafanikio lazima kuwe na dhamira ya kweli ya kisiasa,” amesema Mbowe.


“Wote ni mashahidi kwamba siku zote viongozi wa CCM waliopo madarakani na wastaafu wameambukizana ugonjwa wa kusema amani. Nikamwomba mama tuhubiri haki, tusihubiri amani,” amesema Mbowe.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad