MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ameendelea kukoleza moto kuhusu kuwapo kwa siasa za kiungwana na kistaarabu zenye misingi ya kudumisha amani, upendo na mshikamano.
Mbowe, jana alifika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Queen Sendiga na kufanya mazungumzo na wawili hao walikubaliana kufanya siasa za kistaarabu mkoani hapo. Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi (ACP) Allan Bukumbi.
Akizungumza baada ya kufanya mazungumzo na Sendiga, Mbowe alisema kama ambavyo alizungumza na Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kutoka gerezani, anaona ni vyema kuendelea kueneza ujumbe wa siasa za kistarabu ili kukuza demokrasia.
"Tulikuwa kwenye mkoa wenu wa Iringa na tumemaliza uwapo wetu kwa usalama ndani ya mkoa huu. Tunashukuru na tumeona ni vizuri kukutana na viongozi wa serikali ya mkoa huu,” alisema.
Mbowe alisema mambo ambayo alizungumza na Rais Samia juu ya kuijenga Tanzania na mambo ambayo yanapaswa kuzungumzwa kila wakati na kila mmoja wetu kuona siasa zonazofanyika zinakuwa za kistarabu na zenye upendo na mshikamano badala ya kufanya siasa za ugomvi na uhasama.
Kiongozi huyo alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Sendiga, kwa kukubali kumkaribisha ofisini kwake na kufanya nae mazungumzo hayo.
Sendiga kwa upande wake alimpongeza Mbowe kwa kufika ofisini kwake na kubainisha kuwa ofisi yake ni ya umma, hivyo inampokea kila mmoja na kuwa busara zake za kufika ofisini ni wazi anahitaji taifa lenye siasa safi.
Alisema Mbowe amemwomba kuendelea kufanya siasa safi ndani ya mkoa na yeye kwa nafasi yake ya mkuu wa mkoa, amemhakikishia kufanya siasa safi zenye tija kwa ustawi wa taifa.
Alisema Mkoa wa Iringa utaendelea kudumisha siasa safi zenye maendeleo kwa kuwa suala la amani na utulivu ni msingi mkubwa wa maendeleo ya mkoa na taifa.
"Naamini Mbowe huu ndio mkoa wake wa kwanza kuutembelea na kuja kukutana na mkuu wa mkoa. Niseme ni mwanzo mzuri na sisi mkoa tupo kuona amani inadumishwa," alisema Sendiga.
Hata hivyo, Sendiga aliwaomba viongozi wa vyama vya siasa mkoani Iringa kufanya kazi Kwa ushirikiano kwa kufanikisha kwa pamoja kuujenga mkoa na pale penye changamoto, wasisite kumshirikisha badala ya kukimbilia kwenye mitandao ya kijamii.