Mhariri Abeba Bango Runingani Akimshutumu Putin Kudanganya




Katika kipindi cha matangazo ya moja kwa moja ya habari kutoka Kituo cha Runinga cha Channel 1 cha nchini Urusi, mwanamke mmoja anayefahamika kwa jina la Marina Ovsyannikova ambaye ni mhariri wa chaneli hiyo, amefanya tukio lisilo la kawaida baada ya kuchomoza nyuma ya msoma habari akiwa ameshikilia bango ambalo lilikuwa linapinga kitendo cha nchi yake kuivamia Ukraine.

 

Bango hilo lilisomeka kuwa: “Hakuna vita, simamisha vita, msiamini propaganda,wanawadanganya hapa,” ujumbe ambao ulionwa moja kwa moja na maelfu ya watu waliokuwa wakitazama taarifa hiyo ya habari.

 

Taarifa za habari za kwenye runinga nchini Urusi zinasimamiwa na serikali kiasi kwamba waandishi wa habari wanalazimishwa kuelezea habari nzuri tu kuhusu Urusi katika vita hiyo dhidi ya Ukraine.



Wakati matangazo ya moja kwa moja yakiendelea, sauti ya Marina ilisikika akitamka maneno ya “Hakuna Vita, Simamisha Vita” ambapo msimamizi wa kipindi cha matangazo akalazimika kusimamisha matangazo hayo ya moja kwa moja.

 

Taarifa zinadai kuwa, mapema kabla ya matangazo hayo ya usiku, mwanamke huyo alirekodi video fupi ambayo alilaani kitendo hicho cha Urusi kuivamia Ukraine na kuita uvamizi huo kuwa ni ‘uhalifu’na kusema kuwa anajisikia aibu kufanya kazi katika kampuni ambayo inasambaza propaganda za uongo.

 

Marina katika video yake fupi kabla ya kitendo hicho cha kuingilia matangazo ya moja kwa moja ya runinga alinukuliwa akisema:

“Najisikia aibu kwamba nimehusika katika kusema uongo mbele ya runinga, najisikia aibu kwamba nimewageuza Warusi kuwa watu wa ajabu,” alidai na kuendelea kuwaasa Warusi waandamane kugoma kuendelea kwa vita hiyo na kwamba serikali haitakuwa na uwezo wa kuwaweka wote mahabusu kwani wao pekee ndiyo wenye uwezo wa kumaliza vita hiyo.

 

Imegundulika kuwa Marina Ovsyannikova ana chimbuko la Ukraine kwani baba yake ni raia wa Ukraine na mama yake ni raia wa Urusi.

 

Baada ya tukio na baada ya taarifa zake kufahamika, mwanamke huyo amepongezwa na jumuiya mbalimbali za kimataifa kwa kitendo chake hicho cha kijasiri miongoni mwa walionukuliwa ni Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ambaye amesema anawashukuru sana Warusi ambao bado hawaogopi kusema ukweli, kwa wale ambao wanapambana juu ya taarifa za uongo na wanawaeleza ukweli ndugu na wapendwa wao.

 

Mwanamke huyo mpaka sasa ameshakamatwa na Polisi na yupo mahabusu huku kituo hicho cha habari kikitoa taarifa kuwa kinafanya uchunguzi wa ndani wa kina juu ya tukio hilo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad