KAMA ambavyo zilizuka tetesi za Clatous Chama kurejea Klabu ya Simba kutoka RS Berkane ya Morocco na baadaye ikawa kweli, sinema hiyo imeibuka tena, baada ya kiungo wa zamani wa timu hiyo anayeichezea Al Ahly ya Misri ambao ni Mabingwa wa Afrika, kudaiwa kutaka kurejea tena kwenye klabu hiyo.
Tetesi za Chama aliyeuzwa RS Berkane Agosti mwaka jana zilianza kama mzaha, lakini zilihitimishwa Desemba alipotangazwa kurejea akiwa ameitumikia timu hiyo kwa miezi minne tu.
Klabu ya Al Ahly imetajwa kuwa inaweza kumtoa mchezaji wake raia wa Msumbiji, Miquissone kwa mkopo ili kupisha kusajiliwa mchezaji mwingine wa kigeni, huku Simba ikitajwa kupewa kipaumbele.
Vyanzo mbalimbali nchini Misri vinasema kuwa Kocha Mkuu wa Al Ahly, Pitso Mosimane anatarajia kumtoa kwa mkopo kiungo mshambuliaji wake huyo mwenye umri wa miaka 26, msimu ujao kwa madai ya kushindwa kuelewa mfumo wa ufundishaji wake.
Taarifa zimedai kuwa mwenyewe Miquissone anapendelea kurudi klabu yake ya zamani ya Simba iliyomsajili Januari 2020 kipindi cha dirisha dogo kutoka UD Songo alipokuwa akicheza kwa mkopo, akiwa mali ya Mamelodi Sundowns.
Mchezaji huyo aliyesajiliwa na Mabingwa wa Afrika, Al Ahly Agosti mwaka jana akiuzwa pamoja na Chama, amekuwa hana wakati mzuri ndani ya kikosi hicho ambapo licha ya kwamba amekuwa hapati nafasi ya kucheza, lakini baadhi ya mashabiki na wachezaji wa zamani wa klabu hiyo wanadai ni mchezaji mzuri, lakini siyo wa kiwango cha kuichezea timu kama Al Ahly, na alisajiliwa kwa mihemko tu, baada ya kuifunga bao kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa, Februari 23, mwaka jana kati ya mabingwa hao na Simba likiwa pekee kwenye mechi hiyo Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kama ambayo viongozi wa Simba walivyokuwa wasiri kwenye mkakati wa kumrejesha Chama, wamekuwa wagumu pia kueleza kama wanaweza kumrejesha Miqussone au la kwa mujibu wa taarifa hizo.
Meneja Habari wa Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally alipoulizwa na Nipashe jana, alisema kuwa bado halijamfikia mezani kwake, na kama lipo basi litakuwa juu kwenye uongozi wa klabu hiyo.
“Sijui kama lipo au halipo, linasikikakwenye tetesi, labda kama lipo basi litakuwa kwenye uongozi wangu wa juu, na kama lipo na likawa tayari kwa kuambiwa wanachama na mashabiki, basi watanipa ili niwahabarishe, lakini kama litakuwa ni tetesi, basi litabaki kama tetesi, ila kwa sasa bado kwangu halijafika,” alisema Ahmed.
Viongozi wa Simba kwa miaka ya karibuni wamekuwa wakificha mno mikakati yao hususan ya usajili, kiasi hata suala la Chama lilionekana kama ni tetesi zisizo na mashiko na hekaya za Abunuwasi, lakini lilipofikia tamati likawekwa hadharani.