Misri wakomoa Senegal jijini Cairo katika mkondo wa kwanza wa mchujo wa Kombe la Dunia
Na MASHIRIKA
BAO la dakika ya nne kutoka kwa beki Saliou Ciss aliyejifunga kwa upande wa Senegal lilitosha kuwapa Misri ushindi wa 1-0 mnamo Ijumaa usiku jijini Cairo katika mkondo wa kwanza mchujo wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar mwaka huu wa 2022.
Ciss alibabatizwa na mpira uliopanguliwa na kipa Edouard Mendy kisha kugonga mhimili wa goli baada ya kupigwa na fowadi Mohamed Salah.
Mechi hiyo ilirejesha kumbukumbu za fainali ya Kombe la Afrika (AFCON) iliyoshuhudia Senegal ikizamisha Misri kupitia mikwaju ya penalti baada ya sare tasa mwishoni mwa muda wa ziada mnamo Februari 2022 nchini Cameroon.
Sawa na hali ilivyokuwa Februari, gozi la Ijumaa usiku lilinogeshwa na wavamizi wawili matata wa Liverpool – Salah wa Misri na Sadio Mane wa Senegal.
Vikosi hivyo vitakutana kwa marudiano jijini Dakar mnamo Machi 29, 2022 huku mshindi baada ya mikondo miwili akijikatia tiketi ya kuelekea Qatar kwa fainali za Kombe la Dunia kati ya Novemba na Disemba 2022.
Pharaohs wa Misri watashuka dimbani kwa ajili ya mchuano huo wa mkondo wa pili wakilenga kuendeleza kisasi dhidi ya Lions of Teranga walionyima fursa ya kujizolea taji la nane la AFCON mwanzoni mwa mwaka huu wa 2022 nchini Cameroon.
Hata hivyo, nafuu zaidi kwa Senegal ya kocha Aliou Cisse itakuwa ni kujivunia idadi kubwa ya mashabiki wa nyumbani wakati wa marudiano hayo.