Dar es Salaam. Msanii wa filamu, Yvonne Cherrie, maarufu Monalisa ameeleza maisha yake yalivyokuwa baada ya binti yake, Sonia kukwama Ukraine kwa sababu ya vita vilivyotokana na Russia kuishambulia nchi hiyo.
Vita hiyo imeingia wiki ya tatu sasa, kubwa ikiwa ni Urusi kupinga Ukraine kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi (Nato).
Baada ya kukwama kwa takribani wiki mbili Ukraine, akiwa miongoni mwa wanafunzi wa Tanzania wanaosoma Chuo cha Summy nchini humo, hatimaye wiki iliyopita mtoto wa staa huyo, Sonia alifanikiwa kuvuka mpaka na kuelekea nchini Hungary.
Katika mahojiano na gazeti hili, Monalisa ameeleza namna maisha yake yalivyokuwa magumu katika kipindi ambacho binti yake alikuwa amekwama nchini humo, huku mitandao ya nje ikiripoti kuwa hali inazidi kuwa mbaya.
“Kama mzazi maisha yalikuwa magumu kiasi cha kuathiri mambo yote niliyokuwa nikiyafanya, ikiwamo kazi, kushindwa kula na kutokana na kukosa hamu ya kula nimepungua uzito wa mwili kilo nane nzima.
“Kiukweli nilikuwa nikiishi kwa mawazo sana, chakula wala sikukitamani, nadhani hii ndio moja ya vitu vilivyochangia kunipunguza hata uzito wangu, kwani awali kabla ya sakata hili la vita nilikuwa nina kilo 76 na sasa ninazo 68,” alisema.
Hata hivyo Monalisa alisema anashukuru kwa yote, kwani kila linalotokea lina sababu, kikubwa mtoto wake katoka nchini humo salama.
Alisema kutokana na misukosuko aliyopitia katika kipindi cha wiki mbili, ameamua kwanza akae nchini Hungary kwa mapumziko.
“Amepitia mambo mengi akiwa an umri mdogo, nimekubaliana naye acha abaki nchini Hungary apumzishe akili, kuliko kuanza msukosuko wa kurudi nyumbani, atulie kwanza,” alisema.
Alisema anamuacha atulie na yeye akituliza akili ili aamue binti yake atasoma nchini au nje ya nchi kwa sababu mpaka sasa hajui aamue nini.
“Mapema mno kujua ninataka Sonia asome nje au hapa nchini, najipa muda kwanza maana nilikuwa ninawaza mambo mengi moyoni mwangu wakati binti yangu akiwa katika ardhi yenye vita inayotumia silaha kali, yakiwamo makombora,” alisema.