YANGA imegeuka wodi ya wagonjwa. Wachezaji wanapishana kwenye matibabu kuliko hata uwanjani. Inatia huruma kweli. Kuna tatizo mahali.
Wakati Yanga inakwenda kucheza na Geita Gold wikiendi iliyopita, wachezaji 10 walikuwa majeruhi. Ni karibu kikosi kizima. Bahati mbaya zaidi wengi ni wachezaji muhimu. Ilianza tu kama masihara mwanzoni mwa msimu. Aliumia Yacouba Sogne akapelekwa Tunisia kutibiwa. Baada ya matibabu tukaambiwa atakaa nje ya uwanja kwa msimu mzima.
Baadaye akaumia David Bryson.
Wakati Bryson akisubiriwa apone, wakaumia Kibwana Shomary na Yusuph Athuman. Tukaambiwa kuwa watakwenda kutibiwa nje ya nchi. Mpaka leo Kibwana bado hajarejea uwanjani.
Baadaye akaumia Yassin Mustapha. Ikafikia hatua Yanga ikakosa kabisa beki wa kushoto. Wote walikuwa wodini wakiuguza majeraha. Nani anajali? Nafasi yao akaanza kuchezeshwa Farid Musa. Kocha wa Yanga, Nasredine Nabi hakuwa na chaguo jingine katika nafasi hiyo. Kwa kifupi wachezaji wengi wa Yanga wamepatwa na majeraha na wakakosekana kwa wakati fulani. Namba yao ni kubwa mno.
Bahati mbaya hili halizungumzwi kwa kuwa Yanga inashinda mechi. Wachezaji wanaumia mno.
Nini tatizo? Hili ndio jambo ambalo mashabiki wa Yanga hawaambiwi. Kuna sehemu pana tatizo pale Yanga na ndiyo sababu wachezaji wake wanaumia ovyo.
Kwanza, inawezekana kitengo cha matibabu hakifanyi kazi vizuri ama kina uwezo mdogo. Pili, inawezekana kocha wa mazoezi ya viungo na utimamu wa mwili hayupo vizuri. Programu zake zinawaumiza wachezaji au kocha mkuu ana mazoezi magumu ama wachezaji wanapigana misumari.