Dar es Salaam. Mtoto mkubwa wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu nchini, marehemu Reginald Mengi amefungua maombi Mahakama ya Rufani akitaka ipitie upya uamuzi wake wa kutupilia mbali hoja zao za kutaka mahakama hiyo isisikilize shauri lililofunguliwa na mjane wa tajiri huyo, Jacqueline Ntuyabaliwe anayepinga kutenguliwa kwa wosia wa mume wake.
Machi mwaka jana, Mahakama Kuu, Dar es Salaam, ilitengua wosia wa mwisho wa Mengi baada ya kuyakataa maombi yaliyofunguliwa na watu wanne waliokuwa wakitaka mahakama hiyo iwathibitishe kuwa wasimamizi wa mirathi ya mfanyabiashara huyo.
Mtoto huyo wa Mengi, Abdiel na kaka wa tajiri huyo, Benjamin Mengi walipinga maombi hayo wakidai wosia huo uliompa Jacqueline karibu mali zote za mfanyabiashara huyo haukuwa halali.
Jaji Yose Mlyambina alikubaliana na watoto wa Mengi na kutengua wosia uliodaiwa kuandikwa na baba yao.
Katika wosia huo, Mengi ambaye alikuwa mmiliki wa kampuni za IPP alidaiwa alimrithisha mali zake zote Jacqieline na watoto pacha aliozaa naye---Jayden Kihoza Mengi na Ryan Saashisha Mengi na kuwaweka kando watoto aliozaa na mke wake wa kwanza, Mercy Mengi ambaye walitengana. Mercy alifariki dunia Novemba 2018.
Mahakama Kuu ilikubaliana na hoja za watoto wakubwa wa Mengi kuwa baba yao alikuwa amepoteza uwezo wa kiakili wa kuandika wasia halali kutokana na matatizo ya kiafya yaliyokuwa yakimkabili.
Mahakama hiyo iliridhika kulikuwa na ushahidi wa kutosha kwamba marehemu alipatwa na ugonjwa wa kiharusi tangu Oktoba 2016 na hakupata nafuu hadi mauti yalipomfika.
“Hii ina maana kuwa uwezo wake wa kufikiri na kufanya maamuzi sahihi uliathirika na kumfanya asiweze kuelewa maana ya uamuzi sahihi wa usimamizi wa mirathi yake,” ilisema mahakama.
Vita mpya ya mirathi
Kutokana na uamuzi huo, Jacqueline alifungua maombi Mahakama ya Rufani akiitaka ipitie upya na iubatilishe uamuzi wa Mahakama Kuu wa kutengua wosia wa mume wake uliomilikisha karibu mali zote za tajiri huyo.
Hatua hiyo haikufawafurahisha watoto wa Mengi ambao waliweka pingamizi wakitaka mjane huyo asisikilizwe. Katika moja ya hoja zao, walidai Jacqueline hakuwa na uhalali wa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kwa njia ya kuomba mapitio Mahakama ya Rufani badala ya kukata rufaa.
Pia walidai maombi hayo hayakuwa sawa kisheria kwa kutoambatanishwa na nyaraka muhimu.
Hata hivyo, Mahakama ya Rufani iliyatupilia mbali mapingamizi hayo ikisema kwa kuwa Jacqueline hakuwa sehemu ya kesi ya msingi iliyofunguliwa Mahakama Kuu alikuwa na uwezo wa kufungu mapitio katika mahakama hiyo.
Wakasema hata mapungufu yaliyoainishwa kwenye maombi yake hayakuwa na athari katika kesi aliyofungua, hivyo kutoa kibali kwa shauri alilofungua kusikilizwa.
Watoto wa Mengi wapinga
Hivi karibuni, Abdiel na Benjamin wamefungua maombi katika Mahakama ya Rufaa wakitaka mahakama hiyo ya juu nchini ipitie upya uamuzi wake.
Wanapinga uamuzi wa Mahakama ya Rufani kutupilia mbali pingamizi lao dhidi ya maombi ya mapitio yaliyofunguliwa na mjane huyo akipinga hukumu ya Mahakama Kuu, iliyoukataa wosia huo.
Pamoja na mambo mengine, kina Abdiel katika maombi yao hayo wanadai kuwa uamuzi huo wa mahakama hiyo hauzingatia misingi ya kisheria.
Mawakili wa Jacqueline wameiomba mahakama izitupilie mbali hoja hizo wakidai hazina mashiko kisheria.
Tayari Mahakama ya Rufani imesikiliza hoja za watoto wa Mengi na ndugu zao na itatoa notisi ya kuzijulisha pande zote tarehe ya uamuzi.
Mengi alifariki dunia Mei 2, 2019 akiwa nchini Dubai alipokuwa anapatiwa matibabu.