Mwanamuziki nchini Tanzania Angel Mary Kato, amesema kwamba amewahi kujaribu kujiua kama mara nne, kutokana na changamoto ya matatizo ya afya ya akili yaliyosababishwa na malezi na matarajio ya kuwa na mafanikio fulani.
Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza kwenye kipindi cha MadiniDotCom.
"Maisha yangu yote tangu nikiwa mdogo nilikuwa napambana sana na 'mental health', kwahiyo nikipiga mahesabu nimeshajaribu kujiua kama mara nne hivi, na nilianza kuwaza kujiua nikiwa darasa la 5, kwa sababu tangu nikiwa mdogo tulikuwa tunaishi maisha mazuri na Mama na alikuwa na kazi nzuri, baadaye akatuambia analeta Baba wa kambo na alivyokuja tu kwenye familia alituvuruga sana,walikuwa wanapigana kila siku na Mama", amesema Angel
Aidha Angel ameongeza kuwa, "Mara yangu ya nne kutaka kujiua ilikuwa Septemba 2018, na nilitafuta njia ya kujiua vizuri na ilikuwa baada ya BSS nikijua kwamba maisha yatabadilika, kwa sababu kabla ya BSS tulikuwa na mgogoro wa career mimi na mama, na familia ilinitenga na nilitafuta njia ya kujiua ambayo ni rahisi na isiyokuwa na maumivu,".
Mwanamuziki huyo amesema kwamba, ili kusaidia watu wenye matatizo ya afya ya akili kitu muhimu kinachotakiwa ni kuwapa msaada wa kuwasikiliza na kuzungumza nao na kuwapa moyo na sio pesa