Dar es Salaam. Kiongozi wa jopo la mawakili waliokuwa wakimtetea Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu, Peter Kibatala ameeleza furaha yake baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kufuta kesi iliyokuwa ikiwakabili wateja wao na kuwaachia huru.
Akizungumza leo Machi 4 nje ya Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi jijini Dar es Salaam, Kibatala amesema walifika mahakamani hapo wakiwa wamejiandaa kwa ajili ya utetezi.
“Leo Mkurugenzi wa Mashtaka nchini kwa kutumia madaraka yake aliyopewa na sheria inayoongoza namna ya kuendesha kesi za Jinai nchini amewasilisha mahakamani hati ya nia ya kutoendelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa wote.
“Mnakumbuka walikuwa wanashtakiwa kwa makosa mbalimbali chini ya mwamvuli wa uhujumu uchumi lakini makosa yenyewe yalikuwa makosa yanahusu ugaidi. Mtakumbuka kwamba shauri hilo lilikuwa limepangwa leo kwa ajili ya utetezi.
“Sisi tulikuwa tumejipanga kwa ajili ya utetezi, kwa hiyo sisi tunafurahi kwa hatua hiyo tulitimiza wajibu wetu kwa kadri ya Mungu alivyotuongoza wote. Ambao mlifuatilia mliona kwamba tulifanya kila kile ambacho Mungu ametujalia katika ujuzi wa sheria. Nchi nzima na dunia nzima imeona sisi tunafurahi kwa sababu yetu na kwa sababu ya kazi ya mikono yetu” Kibatala