Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Hamza Johari amesema ndege aina ya Embraer 190 (5H-FJH) iliyozuiwa nchini haiwezi kutumika kulipa madeni ya waliokuwa wafanyakazi wa Fastjet Tanzania kwa sababu haikuwa mali ya shirika hilo.
Johari aliyasema hayo baada ya waliokuwa wafanyakazi 105 wa Fastjet Tanzania, kuingiwa hofu iwapo Sh5 bilioni wanazodai shirika hilo zitalipwa, baada ya kile walichodai kuwa ndege hiyo iliyokuwa imezuiwa kama dhamana, imebadilishwa usajili na kuruhisiwa kuondoka.
Fastjet ilisitisha huduma zake nchini mwaka 2018 huku wafanyakazi wakiwa wanadai baadhi ya stahiki zao, jambo ambalo lilifanya ndege aina ya Embraer 190 (5H-FJH) iliyokuwa inatumiwa na kampuni hiyo kuzuiwa kuondoka nchini kwa amri ya mahakama hadi fedha zinazodaiwa zitakapolipwa.
Mmoja wa waliokuwa wafanyakazi hao, Mummy Katolila aliliambia Mwananchi kuwa ndege hiyo imeonekana imefutiwa usajili wa Tanzania na kuwa tayari kuondoka nchini muda wowote, bila wafanyakazi hao kulipwa stahiki zao.
Alisema Machi mwaka huu ndege hiyo iliruhusiwa kubadilisha usajili wake na kuruhusiwa kuondoka nchini kwa sababu bado inatumika na kampuni mama ya Fastjet PLC, ambayo bado inafanya kazi katika nchi za Afrika Kusini na Zimbabwe.
“Jambo hilo lilifanya sisi tuliokuwa wafanyakazi wa fastjet kukosa matumaini ya kulipwa stahiki zetu, Tunamuomba Rais aitake TCCAA isiruhusu ndege hiyo kuondoka nchini hadi sisi tuliokuwa wafanyakazi tutakapolipwa stahiki zetu,” alisema Mummy.
Akizunguzia suala hilo, Mkurugenzi TCCAA alisema ndege hiyo bado ipo nchini kwa sababu inadaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), lajkinisi kwa ajili ya kulipa wafanyakazi.
“Ndege hii si mali ya Fastjet. Fastjet waliikodi, hivyo mwenyewe akiitaka inarudi. Hivyo ni vyema wafanyakazi waendelee kufuatilia madai yao kwa mufilisi, mali zilizokuwa za shirika hilo zitakapouzwa ndipo watalipwa,” alisema.
“Lakini kama wanadhani wanaweza kulipwa kwa ndege hiyo, haiwezekani, siyo si mali ya Fastjet ni ya kukodi, mwenyewe anaitaka akimaliza deni lake TRA anapewa,” alisema Johari.
Kuhusu kubadilishwa usajili, alisema si kweli ila kilichokuwa kimefanyika ni kubandika ‘sticker’ katika namba za usajili ambayo imebanduliwa na inasomeka kama awali.
Awali alipokuwa akifafanua madai ya wafanyakazi hao, Mummy alisema baada ya Fastjet kusitisha huduma mwishoni mwa mwaka 2018 wafanyakazi walipeleka shauri mahakamani kuomba ndege hiyo kuzuiwa kuondoka nchini hadi watakapoliwa na shirika mama , Fastjet PLC ya Afrika Kusini.
“Mwishoni mwaka 2019 zuio hilo la ndege lilitoka na baada ya miezi, zuio lilifika ukomo na mfilisi wa fastjet alikuwa ameteuliwa na Mahakama Kuu divisheni ya biashara, hivyo wafanyakazi hatukuweza kuendelea na kesi zetu katika mahakama zote.