Dar es Salaam. Baadhi ya wasomi wamesema wanaamini Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Nehemia Mchechu aliliboresha shirika hilo na kuendeleza miradi inayosuasua.
Mchechu, aliyewahi kushika wadhifa huo kwenye shirika hilo aliondolewa Juni 20 mwaka 2018 na nafasi yake kuchukuliwa na Dk Maulid Banyani, aliyeondolewa kwenye wadhifa huo Machi, 14, 2022.
Baadhi ya wasomi waliliambia Mwananchi kuwa uteuzi huo utalipa uhai tena shirika hilo ambalo miradi mingi iliyoanzishwa wakati wa utawala wa Mchechu inasuasua.
“Maana hadi sasa miradi kadhaa, ikiwemo ile ya Kawe na Morocco imesimama na hakukuwa na matumaini yoyote ya kufufuliwa. Lakini liwe fundisho kwa wanasiasa wetu wanapokuwa madarakani kuwa uendeshaji wa mashirika makubwa ya Serikali unahitaji watu wenye weledi wa kazi na siyo taaluma pekee,” alisema Dk Faraja Kristomus, ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Aliwataka viongozi wa Serikali kutambua kwamba sio kila mwanataaluma aliyebobea katika fani yake anaweza kuwa msimamizi mzuri wa mashirika au taasisi za Serikali.
“Hata hivyo, mazingira ya biashara ya majengo huenda yasiwe rafiki kwa sasa tofauti na kipindi chake cha mwanzo. Lakini bado matumaini ya kufufua biashara ya majengo yapo na kutokana na uzoefu wake mkubwa katika eneo hilo ataweza kubadilisha NHC na biashara yake ya majengo,” alisema Dk Kristomus.
Wakili wa kujitegemea, Dk Onesmo Kyauke alisema baada ya Mchechu kuondolewa NHC baadhi ya miradi aliyoianzisha katika mikoa mbalimbali, ikiwemo ya Morocco na Kawe ilikwama.
“Sijui sababu zilizomfanya aondolewe NHC mwaka 2018, lakini jamaa (Mchechu), ana brain nzuri ya kubuni miradi na kuisimamia, nina uhakika ataikamilisha miradi,” alisema Dk Kyauke.
Naye mtaalamu wa uchumi, Oscar Mkude alisema ilionyesha wazi kuwa baadhi ya vitu vilikuwa haviendi tangu alipoondolewa Mchechu.
“Nina uhakika hata baadhi ya miradi aliyoiacha ataikuta haijaendelezwa, sina shaka na utendaji kazi wa Mchechu, ni kiongozi anayeweza kutekeleza majukumu yake endapo akipata ushirikiano wa kutosha serikalini. Tumeona mwanga mzuri kutoka Serikali baada ya NHC kuruhusiwa kukopa,” alisema Mkude.
Alifafanua kuwa Mchechu ni kiongozi mwenye haiba ya kibiashara, akisema jambo hilo alifanikiwa baada ya kuibadilisha NHC, ikiwemo kuanzisha miradi katika mikoa mbalimbali. Alisema katika utendaji kazi wake Mchechu alifanikiwa kuitangaza na kuipandisha NHC.
“Alifanikiwa kufanya maboresho makubwa ya nyumba za shirika ambazo baadhi zionekana kama magofu. NHC lilikuwa linakwenda kibiashara zaidi hasa kupitia miradi mikubwa aliyoianzisha katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Arusha,” alisema Mkude.
Mkude alisema Mchechu anaweza kuirudisha NHC katika ubora kulingana na hali ya uchumi itakavyokuwa. Hata hivyo kuna kila dalili za hali ya uchumi kuanza kuchangamka.
Machi 8, mwaka huu, Serikali iliruhusu NHC, kukopa Sh173.9 bilioni kwa ajili ya kukamilisha miradi mitatu mikubwa iliyokwama kwa miaka minne kutokana na ukosefu wa fedha.Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja Morocco Square na Plot 300 Regent Estate.
Desemba 16, 2017 aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi alimsimamisha kazi Mchechu kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali na Juni 20, 2018 Lukuvi alitengua uteuzi wa Mchechu.