Ni vita ya Mo Salah, Mane leo
IKIWA zimepita siku 47 tangu Senegal iifunge Misri kwenye fainali ya Afcon, timu hizo zinakutana tena leo kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Dunia Qatar 2022.
Senegal na Misri zilipenya kwenye mchujo wa makundi wa kutafuta timu 10 za Afrika zitakazochuana kupata timu tano zitakazowakilisha bara hilo, kwenye michuano hiyo mikubwa duniani.
Mchezo wa kwanza baina ya timu hizo utapigwa Uwanja wa Cairo, Misri majira ya saa 4:30 usiku na marudiano utapigwa Uwanja wa Abdoulaye Wade, huko Senegal mnamo Aprili 29, mwaka huu.
Mechi hiyo ni kivutio kutokana na ushindani uliopo baina ya nyota wa Senegal, Sadio Mane na kinara wa Misri, Mohamed Salah ambao wote wanakipiga Liverpool ya England.
Ni wazi kuwa michuano ya Kombe la Dunia mwakani itamkosa moja ya nyota hao, kwani timu moja pekee baada ya matokeo ya jumla itaungana na washindi wengine wanne kuiwakilisha Afrika.
Timu zote zimekuwa na mwendo mzuri kwenye mechi zao za mwisho za makundi, ambapo Misri imeshinda mechi nne na sare mbili wakati Senegal ikishinda mechi tano na sare moja.
Licha ya ushindani mkali kila kukicha wa mataifa yao, lakini nyota hao wawili wamekuwa wakifarijiana kila inapotokea mmoja ameshindwa kufikia lengo, kama vile Mane alipowazuia wenzake wa Liverpool kumkaribisha kwa shangwe aliporejea kutwaa Kombe la Afcon, kwa sababu ya kutotaka Salah ajisikie vibaya.
Hilo linetegemewa kuteka hisia za wengi kwa namna nyota hao watakavyofarijiana pia baada ya kumalizika kwa mechi hizo mbili na mshindi kujulikana baina yao.
Mbali na mechi hiyo pia leo kutapigwa mechi nyingine kali zitazoikutanisha Mali dhidi ya Tunisia, Cameroon itapambana na Algeria wakati Ghana ikiivaa Nigeria. DR Congo iliyomaliza kinara wa Kundi J, kundi iliyokuwemo Tanzania pia, itapepetana na Morocco.