WAKATI mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba wakianza rasmi kujiwinda kwa mechi za mzunguko wa pili wa ligi hiyo, kabla ya kuialika RS Berkane ya Morocco kwenye mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Pablo Franco, amesema kazi ni moja ...
tu kusaka "pointi tatu".
Simba ilirejea nchini juzi baada ya kutoka kucheza mechi mbili ugenini za Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USGN ya Niger na kutoka sare ya bao 1-1 kabla ya kwenda Morocco na kuangukia kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya RS Berkane.
Hata hivyo, Simba ambayo ina pointi nne sawa na USGN huku Berkane ikiwa kileleni na alama zake sita na Asec Mimosas ikiburuza mkia kwa pointi tatu, imekuwa timu ya kwanza katika Kundi lao la D, kuambulia pointi ugenini, kwani timu zote zimekuwa zikishinda nyumbani tu na kupoteza ugenini.
Kesho majira ya saa 1:00 usiku miamba hiyo ya Ligi Kuu Bara, itashuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuikaribisha Biashara United katika mchezo wao wa kwanza katika mzunguko huu wa pili.
Simba ambayo ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 31, 11 nyuma ya vinara Yanga walioko mchezo mmoja mbele, baada ya mechi hiyo ya kesho, Jumatatu itashuka tena uwanjani hapo kuikaribisha Dodoma Jiji FC.
Akizungumza na mwandishi wetu jana, Pablo alisema nguvu na akili zao zote sasa wanazielekeza katika mechi hizo mbili za Ligi Kuu ili kuhakikisha wanaondoka na alama zote sita kabla ya kuikaribisha RS Berkane Machi 13, mwaka huu.
Pablo alisema anatarajia mchezo huo utakuwa mgumu hasa kutokana na ubora wa Biashara United, lakini pia imekuwa kawaida kwa timu ndogo kutoa ushindani mkubwa zinapocheza na timu kubwa.
"Biashara ni timu nzuri na inacheza kitimu, lakini ina wachezaji wazuri na inapocheza na timu kubwa inatoa ushindani mkubwa, lakini kikubwa kwetu ni kuhakikisha tunapata ushindi na uzuri ni kwamba tutakuwa nyumbani," alisema kocha huyo raia wa Hispania.
Alisema malengo yao ni kuhakikisha wanashinda mechi zao ili kupunguza pengo kubwa la pointi kutoka kwa timu inayoongoza kwenye msimamo wa ligi hiyo, Yanga ili kuweza kutetea taji lao msimu huu.
Kauli hiyo ya Pablo haikutofautiana na ya nahodha wa kikosi hicho, John Bocco, ambaye naye alisema akili zao wamezihamishia katika michezo hiyo miwili kabla ya kuikaribisha RS Berkane mwishoni mwa wiki ijayo.
Bocco alisema tayari wameona tofauti kubwa dhidi ya Yanga walioko kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo na kikubwa kwao ni kuendelea kushinda kila mchezo hadi mwisho wa msimu.
"Tumeona tofauti kubwa ya pointi dhidi ya timu inayoongoza ligi, hivyo kwa sasa tunahitaji kushinda mechi zetu ili kuendelea kuzipunguza na kutoa presha kwao ili kutimiza malengo yetu ya kutetea ubingwa," alisema Bocco ambaye kwa sasa 'gari' limewaka kwake baada ya kuanza msimu kwa ukame wa mabao.
Katika mechi hiyo, Simba imewaeleza mashabiki wake watarajie kuona baadhi ya wachezaji ambao walikuwa majeruhi wa muda mrefu, wakipata nafasi baada ya kuwa fiti kwa sasa.
Wachezaji ambao walikuwa majeruhi ni pamoja na kiungo mkabaji Taddeo Lwanga, ambaye kwa muda sasa amekuwa akifanya mazoezi ya pamoja na kikosi cha kwanza.