Paul Makonda "Nipo Tayari Kutoa Ushiriakiano Kwa Polisi"



KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu, leo Machi 12, 2022 amezungumza na waandishi wa habari na kueleza muhtasari wa kilichojadiliwa katika kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM kilichofanyika.

Miongoni mwa mambo aliyoyazungumza Shaka, amewaambia waandishi wa habari kwamba kamati kuu imeaiagiza serikali kulifanyia uchunguzi wa kina jeshi la polisi kutokana na kuwepo kwa matukio mengi ya baadhi ya askari kuvunja sheria na maadili ya kazi zao na kusababisha uonevu kwa raia.

Muda mfupi baada ya taarifa hiyo ya Shaka kusambaa, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ameibuka kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram na kueleza kuwa anaunga mkono suala la polisi kuchunguzwa kwa sababu wapo wanaoshirikiana na wafanyabiashara matapeli.

Makonda ameandika: “Naunga mkono hoja ya Kamati Kuu ya kuchunguza mwenendo wa baadhi ya maafisa wa jeshi la polisi, wanaolipaka tope jeshi la polisi kwa kuwalinda wafanyabiashara matapeli wanaodhulumu mali za watu.


“Naomba tuanze na Dar es Salaam na mimi Paul Makonda nipo tayari kutoa ushirikiano.”

Ujumbe huo wa Makonda umezua gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii, hasa ikizingatiwa kwamba, mkuu huyo wa mkoa wa zamani, anatajwa kuwa kwenye mgogoro na mfanyabiashara mkubwa ambaye pia ni mdhamini wa Klabu ya Soka ya Yanga, Ghalib Said Mohamed (GSM).

Makonda na GSM, wameingia katika mvutano mkubwa, wakigombea kiwanja ambacho ndani yake kumejengwa nyumba ya ghorofa ambayo haijakamilika, Makonda akidai kiwanja na nyumba hiyo ni mali yake huku GSM kupitia kwa wanasheria wake, wakidai kwamba yeye ndiye mmiliki halali na anazo nyaraka zote muhimu.


Mapema asubuhi ya leo, Mwanasheria wa GSM, Alex Mgongorwa aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza kwamba mtu yeyote ambaye ana vielelezo vyinavyoonesha kwamba kiwanja kinachogombewa ni chake, basi ajitokeze katika vyombo vinavyohusika.

Makonda na GSM wanagombea kiwanja namba 60 kilichopo mtaa wa Regent Estate eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad