Rais Joe Biden wa Marekani amesema madikteta ambao hawawajibishwi kutokana na uchokozi wao ndio wanaosababisha machafuko zaidi duniani.
Rais Joe Biden wa Marekani amesema madikteta ambao hawawajibishwi kutokana na uchokozi wao ndio wanaosababisha machafuko zaidi na kuongeza kuwa uvamizi wa rais Vladimir Putin wa Urusi nchini Ukraine ulikuwa ni wa kupangwa na wala haukuchochewa.
Rais Biden ameyasema hayo kwenye hotuba ya hali ya taifa aliyoitoa kwa bunge la Marekani. Biden amegusia pia umuhimu wa washirika wake wa Ulaya akisema muungano ulioanzishwa baada ya Vita vya Pili vya duniani ili kurejesha amani na ustahmilivu una umuhimu mkubwa pia katika kipindi hiki na kusema Putin alikosea sana kuamini angeweza kuugawanya ushirikiano wa NATO, kwa kukataa juhudi za kidiplomasia.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock kwa upande wake ametoa mwito kwa mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa kuunga mkono azimio la kulaani uvamizi huo wa Urusi, akisema ni wakati sasa wa kuchagua kati ya amani ama uvamizi, haki ama matakwa ya wenye nguvu, kuchukua hatua ama kufumbia macho. Amesema hayo kwenye mkutano wa dharura wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.
Aidha balozi wa Urusi kwenye Umoja huo Gennady Gatilov amesemaUkraine haina nia ya kujaribu kusaka suluhisho halali na la usawa kuhusiana na mzozo baina yao. Amesema hayo akiwa mjini Geneva, kwenye mahojiano na kituo cha televisheni cha nchini Lebanon.
Kampuni ya Apple imetangaza kusitisha biashara zake nchini Urusi kufuatia uvamizi wake nchini Ukraine
Shrika la habari la Urusi la RIA, lilimnukuu Gutilov kwenye mahojiano hayo akisema Urusi inaunga mkono diplomasia na usawa, lakini kwa sasa hawalioni hilo na kuongeza huu ni wakati muafaka wa kondoa silaha za nyuklia mashariki na magharibi mwa Ulaya.
Mbali na Urusi, wanajeshi wa mataifa mengine yenye nguvu kinyuklia barani Ulaya, Ufaransa na Uingereza pamoja na Marekani, ambayo pia yanamiliki silaha nyingi za nyuklia miongoni mwa wanachama wa NATO wamepiga kambi barani Ulaya.
Mapema leo Umoja wa Ulaya, umezuia mashirika ya habari ya Urusi ya RT na Sputnik kutangaza kutokea eneo la umoja huo, baada ya mtandao wa Youtube kuzuia maudhui ya mashirika hayo kwenye Umoja huo. Hatua hii inayotarajiwa kuanza kutekelezwa hii leo baada ya kuchapishwa kwenye jarida rasmi la Umoja huo.
Wawakilishi wa mataifa 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya aidha wamekubaliana kuzizuia baadhi ya benki za Urusi kutumia mfumo wa benki wa SWIFT.
Kampuni ya teknolojia ya Apple imetangaza kusimamisha uuzaji wa simu zake za iPhone, kompyuta na vifaa vyake nchini Urusi. Kwa kufanya hivyo, Apple inakuwa kampuni ya karibuni kutangaza kuondoa bidhaa zake kwenye soko la Urusi. Kampuni hiyo imesema wana wasiwasi mkubwa kuhusu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na inasimama na watu wanaoteseka kutokana na machafuko.