Rais Samia Afunga Mjadala wa Tundu Lissu



​​​​​​​RAIS Samia Suluhu Hassan amevunja ukimya kuhusu suala la usalama wa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, huku akisema akirejea nchini ataishi kama Watanzania wengine wanavyoishi.

Rais Samia alitoa kauli hiyo juzi wakati akihojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuhusu mwaka mmoja wa uongozi wake tangu aingie madarakani baada ya kifo cha mtangulizi wake, Hayati Dk. John Magufuli. Magufuli alifariki dunia Machi 17, mwaka jana.

"Nimhakikishie usalama wake kwani ana wasiwasi gani? Kwani nani hana usalama ndani ya nchi? Sisi sote tumo humu ndani tuko salama. Akirudi ataishi kama Watanzania wengine wanavyoishi,” alisema Rais Samia baada ya kuulizwa na mtangazaji kuhusu ombi la Lissu kuhakikishiwa usalama atakaporejea nchini.

Kauli hiyo ya Rais Samia imemaliza mzizi wa fitina juu ya maombi ya mara kwa mara ya Lissu ambaye kwa sasa anaishi nchini Ubelgiji. Lissu amekuwa akiitaka serikali impe hakikisho la usalama wake atakaporejea nchini.

Alipoulizwa kuwa wasiwasi wa Lissu kurejea nchini unatokana na watu waliomshambulia hawajapatikana na bado uchunguzi haujakamilika, Rais Samia alisema: “Uchunguzi wa tukio lake utakamilikaje wakati yeye hayupo? Inapaswa yeye arudi. Yeye ndiye mhusika, hivyo lazima awapo ili hao wanaofanya uchunguzi ashirikiane nao."


Kuhusu alipofanya mazungumzo na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, baada ya kutoka gerezani kama kulikuwa na suala la kuombana radhi kwa yaliyotokea, alisema hakukuwa na suala kama hilo.

Hata hivyo, alisema walichozungumza ni kupiga mstari mwekundu matukio yaliyopita na kuyaweka kando na sasa jambo la msingi lililobaki ni kujenga nchi.

"Nani kamwomba radhi mwenzie? Hapa hakuna kuombana radhi. Tulizungumza kwamba tunapiga mstari mwekundu yaliyopita yamepita twende tukajenge nchi yetu," alisema.


Kuhusu kesi ya Mbowe kama itakuwa imetia doa utawala wake na kauli aliyowahi kuitoa wakati kesi ikiwa bado inaendelea mahakamani, Rais Samia alisema haijatia doa lolote wala kuleta ugumu kwa mahakimu na majaji kwa kuwa uongozi wake ni wa utawala wa sheria.

"Haikutoa wakati mgumu kwa sababu kile (mahakama) ni chombo pekee na ni mhimili unaofanya kazi kwa kujitegemea. Kwa hiyo nitakachosema mimi wala hakiwaathiri wao chochote. Mhimili wenyewe umekaa umefanya kazi zao basi," alisema Rais Samia
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad