Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amekitaka Kikosi Kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi nchini kuja na mapendekezo ya mchakatako wa Katiba Mpya, Tume Huru ya Uchaguzi pamoja na kukomesha rushwa.
Rais Samia ameyasema hayo leo Machi 21, 2022 wakati akipokea taarifa ya kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi nchini.
"Hili la katiba mpya mtakwenda kulifanyia kazi, mtaleta mapendekezo yatakayotangazwa kwa Watanzania wote waelewe. Mimi nakubaliana kwamba ni jambo la muda mrefu, lakini Watanzania wote waelewe hivyo," amesema Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande mwingine Rais Samia amesema Kikosi Kazi hicho pia kinatakiwa kushughulikia masuala ya rushwa kwenye jamii, Uchaguzi pamoja na masuala mbalimbali ya siasa.
''PCCB haifanyi kazi yake ipasavyo, hili sio la uongo ni kweli ingawa ukisema wenyewe wanakasirika. Ukisema Jeshi la Polisi halifanyi kazi vizuri unakwenda kujibiwa... hatufanyi kazi vizuri, hauamini vyombo vyako?'' - ameeleza Rais Samia.