Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema uzinduzi wa mradi wa daraja la Tanzanite ni sehemu ya kumuenzi Rais wa awamu ya tano, John Magufuli.
Ameyasema hayo leo Alhamisi Machi 24, 2022 Dar es Salaam kwenye hafla ya uzinduzi wa daraja hilo lilogharimu Sh243 bilioni.
Rais Samia amesema Desemba 20/2018 aliyekuwa Rais Hayati Magufuli aliweka jiwe la msingi kwa ajili ya kuanza ujenzi huo na kueleza kwamba ni siku ya furaha kuona kazi aliyoianzisha imekamilika.
“Na tumekusanyika hapa kwa ajili ya uzinduzi na kama nilivyosema mara kwa mara kwamba tutakamilisha kazi zote alizozianzisha kwahiyo kwangu mimi uzinduzi wa daraja hili ni sehemu ya kumuenzi Rais John Magufuli,”amesema
Rais Samia amesema serikali ya Korea Kusini ni mdau mkubwa wa maendeleo ambaye amekuwa akiwaunga mkono katika sekta mbalimbali za kimaendeleo hususan kwenye miundombinu.
“Kwaniaba ya wananchi wa Tanzania napenda kutoa shukrani kwa Jamhuri ya Korea ya Kusini kwa mchango wao mkubwa wa maendeleo katika Taifa letu,”amesema
Amesema ujenzi wa daraja hilo ni muendelezo wa Serikali katika kufanya maboresho kwenye sekta ya miundombinu ili kukabiliana na kero ya msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam.
“Kwa kufanya upanuzi wa barabara za juu na miundombinu ya mabasi yaendayo haraka ili kurahisha usafiri ndani ya jiji la Dar es Salaam,”amesema