Rais Samia "Hakuna Kuulizana Dini Wakati wa Kuchukua Sensa"



Rais Samia Suluhu Hassan amesema hakuna mtu atakayeulizwa dini yake wakati wa sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu. Anaripoti Mwandishi Wetu…

Ameyasema hayo leo tarehe 8 Machi, 2022 wakati wa hotuba yake kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika kitaifa Unguja visiwani Zanzibar.

Rais Samia amesema “kuna propaganda” zinazoenezwa kuwa katika sensa ya mwaka huu watu wataulizwa dini zao, suala ambalo amelikanusha na kuwahakikishia wananchi wote kuwa “hilo halipo.”

Amesema tangu kuanza kwa sensa nchini watu hawajawahi kuulizwa dini zao “nashangaa wale waliozuka na kusema sensa mwaka huu itakwenda kuulizwa watu dini zao.


“Nataka niwahakikishie kwamba suala hilo halipo, tulishakataa toka Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, alitukataza kuulizana dini zenu nini na sensa zote zilizofanyika Tanzania hili halijapata kufanyika,” amesema Rais Samia.

Alifafanua kuwa mabadiliko yatakayokuwepo sensa ya mwaka huu ni kujua anwani za makazi ya kila mwananchi.

“Na tumeanza na hilo (anwani za makazi) ili sensa yetu ikafanyike vema na tuone katika ramani zetu zitakazochukuliwa kidigitali, tuone maeneo ambayo hayajahesabiwa na maeneo ambayo maofisa watayaruka hivyo tunataka kuhakikisha watu wote wanahesabiwa,” amesema.


Aidha aliwataka wananchi kutoa ushirikiano katika suala la anwani za makazi kwasababu litakwenda kusaidia mambo mengi na si tu sensa.

“Dunia inabadilika nasi tubadilike. Biashara sasa zinakwenda kwenye mtandao na zinapokwenda huko ukinunua kitu kinaletwa hadi mahali ulipo kwa kutumia anwani hizo,” amesema Rais Samia.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad