Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan leo amekutana na kufanya mazungumzo na mwanafunzi Emmanuel Mzena, ambaye alimuahidi kumtembelea shuleni kwake, na amemuahidi atamtekelezea yale aliyomuomba ikiwemo kumsomesha nje ya nchi.
Kauli hiyo ameitoa leo Machi 7, 2022, alipofanya ziara katika shule ya Benjamin Mkapa, Jijini Dar es Salaam, na kudokeza mambo mawili muhimu aliyozungumza na mwanafunzi huyo mwenye ulemavu ambaye alimuomba Rais Samia amfungulie taasisi yake yenye lengo la kuwasemea watoto wenye ulemavu wanaofichwa majumbani ili wapelekwe kupata elimu.
"Emmanuel ameniambia, namshukuru sana Mama yangu pamoja na changamoto alizonazo za maisha amejitahidi nimesoma mpaka kufikia hapa, mwaka huu nitafanya mtihani wa kidato cha sita, sina matumaini ya kupata ajira za serikali hivi nilivyo," amesema Rais Samia.
Rais Samia ameongeza kwa kusema, "Lakini nakuomba mama nikimaliza kidato cha sita nisomeshe nje, na la pili nifungulie taasisi yangu mwenyewe, lengo langu ni kuwasemea watoto kama mimi waliofichwa majumbani watolewe waje wapate elimu, hilo ndilo nililoongea na Emmanuel, pamoja na mawili matatu ambayo ni siri yetu, na mimi nikamuahidi nitafanya hivyo,".