Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema Rais wa Afrika kusini, Cyril Ramaphosa amepunguza ushawishi wake kama mpatanishi wa mgogoro wa vita nchini Ukraine akiwa na pendekezo lenye utata kwamba hatua za NATO ndizo za kulaumiwa kwa uvamizi wa Russia dhidi ya jirani yake wa magharibi.
Ramaphosa anasema anapendelea mazungumzo badala ya silaha au vikwazo vya kiuchumi akimaanisha vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Russia kutoka Marekani na washirika wa magharibi baada ya uvamizi huo, ambao sasa ni wiki yake ya nne.
Vita hivyo vingeepukika kama NATO ingezingatia maonyo kutoka kwa viongozi na maafisa wake kwa miaka mingi, kwamba upanuzi wake wa mashariki ungesababisha kukosekana kwa utulivu katika eneo hilo, Ramaphosa aliliambia bunge alhamisi wiki iliyopita.
Lakini aliongeza kuwa Afrika kusini haiwezi kuunga mkono matumizi ya nguvu, na ukiukaji wa sharia za kimataifa. Rais wa Afrika kusini alisema nchi yake iliombwa kuwa mpatanishi katika mzozo huo lakini hakumtaja ni nani aliyeiomba Afrika kusini kuingilia kati.