Roman Abramovich: Mshirika wa Putin Mwenye Nguvu, Utajiri Uliogubikwa na Usiri



Roman Abramovich, bilionea mmiliki wa klabu ya soka ya Chelsea, alikuwa yatima asiye na senti, lakini akainuka kutoka kwenye majivu ya Russia ya Usovieti na kuwa mmoja wa watu matajiri na wenye nguvu duniani.

Hadithi ya maisha yake ya kuvutia imegubikwa na siri kubwa mpaka sasa. Ni tajiri wa Russia ambaye amefanya mapinduzi makubwa katika soka la Ulaya alipoinunua Chelsea majira ya joto ya 2003 na kuanza kushinda mataji mawili ya Ligi Kuu ya England. Kila kipengele cha maisha yake ya zamani, ya sasa na yajayo ni cha kusisimua.

Katika mfululizo wa makala hizi, tutaangazia malezi yake, ikiwa ni pamoja na historia yake ya Kiyahudi, urafiki ambao ulimsaidia kuingia kwenye safu ya juu ya Kremlin, jukumu lake kuu katika kuongezeka kwa matajiri ambao ni watawala wa Serikali ya wachache nchini Russia, mikataba ya biashara iliyomfanya awe tajiri katika muda usiozidi miaka kumi, na kinachomfanya kuwa na jina kubwa katika nchi za Magharibi kama ilivyo katika nchi yake.

Kuna hadithi za kipekee nyuma ya mabilioni ya Abramovich aliyotengeneza nchini Russia kwa mtindo wa ubepari wa nchi za Magharibi uliyoanzishwa na Rais Vladmir Putin. Pia tutaangazia sababu za yeye kuwekeza sehemu ya utajiri huo kwa wababe hao wa soka la England na dunia kwa sasa, Chelsea.


Kuinuka kwa Abramovich kutoka kuwa yatima wa eneo dogo hadi kuwa mmoja wa wanaume wenye nguvu zaidi nchini Russia, ni hadithi ambayo ina viungo vyote vya kusisimua: kujihatarisha, ujasiri, busara, ukatili na juu ya yote ni haiba ya hila na ya ujanja.

Mara ya kwanza umma wa Russia kusikia habari za mwanadamu anayeitwa Roman Abramovich ilikuwa mwaka 1998 alipotajwa kama ‘pochi’ ya Rais Yeltsin kwenye kipindi maarufu cha ‘Itogi’ katika televisheni ya Russia ambacho ni maarufu kwa habari kupitia mchambuzi wa masuala ya uchumi, Yevgeni Kiselev.

Kufikia wakati huu, Abramovich alikuwa tayari bilionea. Habari ya utajiri wake ilipoenea, vyombo vya habari vilianza kuvutiwa naye. Kulikuwa na shida moja tu: jinsi ya kuelezea hadithi kuhusu mtu ambaye alikuwa akijulikana kama mjumbe wa siri wa Serikali ya watu wachache.


Mwishoni mwa mwaka 1999, hakuna gazeti wala kituo cha televisheni kilichokuwa na picha ya Abramovich. Baada ya kutokuwa na picha yake, gazeti moja liliamua kutoa fedha ili kumaliza ‘tatizo’ hilo. Ilitoa zawadi ya kiasi cha rubo (sarafu ya Kirusi) milioni moja kwa mtu yeyote, ambaye angeweza kupata picha yake, hata kama ni ya kuchorwa. Hilo donge nono kwa ajili ya kupata picha yake lilizaa matokeo yaliyotarajiwa. Ingawa picha iliyopatikana ubora wake ulikuwa umefifia, ilitumika kwa miezi kadhaa katika vyombo vya habari vya Russia.

Kwa wakati huo, mshauri wa uhusiano wa umma wa Abramovich, ambaye ni Mwingereza anayeitwa Gregory Barker, na ambaye baadaye alikuja kuwa mbunge wa chama cha Conservative nchini humo (2001–2015), alijaribu kumshawishi apigwe ‘picha nzuri’, lakini alikuwa akikwepa.

Baadaye Abramovich alikuja kupigwa picha na Yuri Feklistov, ambaye ni mpigapicha wa jarida la Ogonyok. Feklistov alifanikiwa kumpiga picha Abramovich kwa hisani ya urafiki wake na Valentin ‘Valya’ Yumashev, mwandishi wa habari ambaye aliandika historia ya maisha ya Boris Yeltsin, Rais wa kwanza wa Shirikisho la Russia kutoka 1991 hadi 1999.

Yumashev na mkewe Tatyana wakageuka kuwa kichocheo muhimu katika ujenzi wa utajiri wa Abramovich na wamekuwa marafiki tangu mwaka 1996. Valya na Yuri, wakati huo huo, wamefahamiana kwa miaka 20 baada ya kwanza kufanya kazi pamoja kwenye gazeti la ‘Komsomolskaya Pravda’ na sasa Feklistov amethibitishwa kama mpigapicha wa Abramovich. Mbali na kumpiga picha nyumbani na kazini huko Moscow, aliandamana naye katika shughuli za kifamilia hadi bilionea huyo alipochaguliwa kuwa gavana mwaka 2000.


Abramovich alizaliwa Jumatatu ya Oktoba 24, 1966. Miezi michache baada ya kuzaliwa, mama yake, Irina, akagundua kuwa ana ujauzito mwingine baada ya kupata mtoto wake wa kwanza, alichagua kutoa mimba. Cha kusikitisha, dawa aliyotumia kuitoa mimba iligeuka sumu iliyomuua akiwa na umri wa miaka 28 tu. Alifariki wakati Roman akiwa hajatimiza hata mwaka mmoja. Baba yake, Aron (Arkady) Abramovich Leibovich naye alifariki mwaka 1969 wakati Roman akiwa na umri wa miaka mitatu. Babu na bibi wa Roman kwa upande wa mama walikuwa ni Vasily Mikhailenko na Faina Borisovna Grutman, wote wakiwa ni Wayahudi waliozaliwa Ukraine. Babu na bibi yake kwa upande wa baba walikuwa ni Nachman Leibovich na Toybe (Tatyana) Stepanovna Abramovich, ambao walikuwa Wayahudi wa Belarus.

Akiwa amepoteza wazazi wote wawili kabla ya kufikisha umri wa miaka mitatu, Abramovich alilelewa na jamaa za wazazi wake huku akiishi na bibi yake mzaa baba katika chumba kimoja jijini Moscow katika mtaa wa Tsvetnoi Boulevard. Pamoja na kuishi na bibi yake, aliyebeba sehemu kubwa ya majukumu ya kumtunza ni mjomba wake, Abramu.

Kutokana na urasimu wa Sovieti, shule ya kwanza ya Abramovich iliitwa kwa kifupi ‘Shule Nambari 2.’ Maneno haya, ‘Lazima usome, usome, usome’ yakiwa yamejengwa kwa zege juu ya lango kuu la kuingilia shuleni, na hayo yalikuwa ni himizo la Vladimir Lenin, kiongozi wa kwanza wa Soviet Russia.

Abramovich alikuwa mwanafunzi wa wastani darasani. Hakuwahi kushinda tuzo zozote za shule, hata mwalimu mkuu wake alikiri kuwa hakuwa na kipawa cha elimu. Lakini, kulikuwa na dalili alikuwa mjanja-mjanja kuliko wenzake waliomzidi kitaaluma. Alikuwa mdadisi sana na mara zote aliuliza maswali mengi.


Mbali na kazi yake ya kitaaluma, alienda mara kwa mara katika safari za shule katika miji kama vile Brest, St Petersburg (wakati huo Leningrad), na Pskov na watu walizungumza juu ya udadisi alioonyesha kwenye safari hizi, kiu yake isiyoweza kutoshelezwa ya ujuzi.

Baada ya miaka tisa ya kufanya kazi kwa bidii na kupata marafiki, Abramovich aliacha shule mwaka 1983.

Je, kwa nini aliacha shule na alipitia mambo gani kwenye maisha yake na ukuaji? Usikose kesho.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad