Makamu wa Rais wa RS Berkane Majid Medrane amethibitisha kuandikwa kwa barua ya malalamiko na kutumwa Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ kuhusu mapungufu yaliyojitokeza kwenye mchezo wa Mzunguuko wanne wa ‘Kundi D’, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Simba SC.
RS Berkane wamemlalamikia Mwamuzi kutoka DR Congo, Jean Jacques Ndala Ngambo aliyechezesha mchezo huo, kwa kigezo cha kushindwa kusimamia vyema sheria 17 za mchezo wa soka kwenye mchezo huo.
Majid Medrane amesema: “Ndiyo Tumeandiika barua, kulikuwa na makosa matano dhidi yetu. Bao la Simba SC halikuwa halali, wachezaji wawli walikuwa wameotea wakati bao linafungwa, Makosa mengine ni kunyimwa penato ya halali.”
“Kukataa bao la wazi tulilofunga , mchezaji wa Simba alistahili kadi nyekundu kwa kumchezea rafu mbaya mchezaji wetu na pia na dakika 10 ziliongezwa lakini hazikuchezwa zote”
Mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam, Simba SC ilichomoza na ushindi wa bao 1-0, lililopachikwa wavuni na Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Senegal Pappe Ousman Sakho na kuifanya Simba SC kufikisha alama 07 kwenye msimamo wa Kundi D.
Nafasi ya Pili kwenye msimamo wa kundi hilo inashikwa na ASEC Mimosas ya Ivory Coast yenye alama 06 baada ya kuifumua USGN mabao 2-1, sawa na RS Berkane inayoshika nafasi ya tatu, huku USGN ikishika nafasi ya 04 kwa kumiliki alama 04.
Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kundi D itaendelea tena mwishoni mwa juma hili (Machi 20), ambapo Simba SC itakua ugenini ikicheza dhidi ya ASEC Mimosas nchini Benin, huku USGN ikiikaribisha RS Berkane mjini Niamey-Niger