Russia yajibu Mapigo ya Vikwazo Ulaya




Moscow. Wakati mataifa ya Magharibi yakiiwekea vikwazo Russia kwa kuivamia Ukraine, nchi hiyo imejibu mapigo kwa kuzuia bidhaa zake muhimu kuuzwa kwa mataifa hayo.

Zuio hilo linahusisha bidhaa za mawasiliano, dawa, magari, kilimo, vifaa vya umeme na bidhaa za misitu na madini adimu.

Wizara ya Uchumi ya Russia pia imesema itazipiga marufuku meli za kigeni kutia nanga katika bandari zake.

“Hatua hizi zinalenga kujibu vikwazo vilivyowekwa kwa Russia,” imesema wizara hiyo.


Imeongeza kuwa, vikwazo vilivyowekwa ambavyo si rafiki vimelenga kutoingilia sekta muhimu za kiuchumi.

Zuio la kutouza bidhaa zake nje ya nchi limehusisha bidhaa zaidi ya 200 na litaendelea hadi mwisho wa mwaka.

Nchi za Magharibi zimeiwekea vikwazo vya kununua mafuta Russia na kwa mabilionea ambao ni watu wa karibu wa Rais Vladimir Putin.


Zuio la Russia linatarajiwa kuziathiri nchi 48 zikiwemo Marekani na za Umoja wa Ulaya. Tangazo la zuio hilo limesema unafuu utaihusu Georgia na eneo la Kusini mwa Ossetia na Abkhazia na nchi wanachama wa Umoja wa Kiuchumi wa Russia.

Waziri Mkuu wa Russia, Mikhail Mishustin alisema zuio hilo litahusisha uuzaji wa bidhaa zilizotengenezwa na kampuni za Russia, yakiwemo magari, mabehewa ya reli na makontena.

Zuio hilo limekuja baada ya hivi karibuni, Rais mstaafu wa Russia, Dmitry Mevedev kuonya kwamba mali zinazomilikiwa na kampuni za nje zitataifishwa na Serikali.

Mali hizo ni pamoja na viwanda vya kutengeneza zana za migodi kama Caterpillar na Rio Tinto Starbucks, Sony, Unilever na Goldman Sachs.


Jumatano iliyopita, Russia ilichukua hatua ya awali ya kutaifisha mali za kampuni za kigeni zilizomo nchini humo.

Katika taarifa yake Medvedev, alisema “Serikali ya Russia inafanyia kazi hatua hizo ikiwa pamoja na kufilisi na kutaifisha mali za mashirika ya kigeni. Kampuni za kigeni zinapaswa kuelewa kuwa, itakuwa vigumu kurudi kwenye soko.”

Aliwashutumu wawekezaji wa kimataifa kwa kutengeneza hofu kwa wananchi wao ambao watapoteza kipato cha maisha yao.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni, Russia ni mshirika mkubwa wa 19 wa kibiashara wa Uingereza na imefanya biashara zenye thamani ya pauni 15.9 bilioni (Sh47 trilioni) hadi kufikia mwisho wa mwaka 2020.


Marekani yaiona China

Wakati huohuo, Marekani imeionya China ikisema itakabiliwa na athari kali endapo itatoa msaada wa uvamizi nchini Ukraine.

Taarifa zinaeleza kuwepo kwa dalili za China kuisaidia Russia.

Hata hivyo, ubalozi wa China mjini Washington ulisema haufahamu ombi hili.

Kwa mujibu wa magazeti ya Financial Times na New York Times ya Marekani, Russia inaitaka China kuipatia silaha za kutumia nchini Ukraine.

Hata hivyo, magazeti hayo hayasemi aina gani ya silaha ambazo Russia imeziomba.


Kutokana na dalili hizo, Marekani imeionya China ikiwa itakubali kuivamia Ukraine.

Onyo hilo limetolewa kabla ya mkutano uliofanyika mjini Rome nchini Italia kati ya maofisa wakuu wa Marekani na China.

Tangu kuanza kwa mzozo huo, China imekuwa ikiunga mkono kejeli kwa Ukraine, lakini haijulikani wazi kama kweli inatoa msaada wowote wa kijeshi au kiuchumi.

Taarifa za vyombo vya habari vya Marekani vimewanukuu maofisa nchini humo wakisema Russia imekuwa ikiomba China vifaa vya kijeshi, zikiwemo ndege zisizo na rubani, lakini jibu la China bado halijulikani.

Akihojiwa na CNN hivi karibuni, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani, Jake Sullivan alisema “kuwasiliana moja kwa moja, au kwa faragha na Beijing kwamba kutakuwa na athari katika juhudi kubwa za kukwepa vikwazo au kusaidia Russia kunarudisha nyuma.

“Hatutaruhusu hilo kutokea na kuruhusu kuwe na njia ya Russia kujiokoa kutokana na vikwazo hivi vya kiuchumi kwa kupata msaada kutoka nchi yoyote, popote duniani.”

Aliongeza kuwa, inawezekana China inafahamu kuwa Putin anapanga kitu kabla ya uvamizi huo kutokea, Beijing, lakini huenda haielewi undani wa suala hilo.

“Kwa sababu inawezekana sana kwamba, Putin aliwadanganya jinsi alivyodanganya wazungu na wengine,” alisema Sullivan.

Sullivan amekutana jana na Yang Jiechi ambaye ni mjumbe wa Baraza Kuu la maamuzi la China, na Mkuu wa Tume Kuu ya Masuala ya Kigeni, mjini Roma.

Ofisa mmoja wa Marekani alidokeza awali kuwa mazungumzo hayo yatajikita katika athari na kutengwa kwa China endapo itaiunga mkono Russia.

Liu Pengyu, msemaji wa ubalozi wa China mjini Washington DC, aliviambia vyombo vya habari vya Marekani kwamba hajasikia ombi hilo la Russia.

“Kipaumbele kwa sasa ni kuzuia hali ya wasiwasi kuongezeka au hatari ya kutodhibitika tena.”

Tangu mgogoro huo ulipoanza, China haijawahi kulaani uvamizi wa Russia nchini Ukraine, ikisema ni masuala halali ya usalama ya Russia na yanapaswa kuzingatiwa kwa uzito.

Vyombo vya habari vya Serikali ya China na maofisa wa Serikali, mbali na kuiunga mkono rasmi Russia, vinasema hiyo ni operesheni maalumu ya kijeshi na si uvamizi.

Wachambuzi wanaeleza kuwa, lengo la Marekani kuikomalia China ni kutaka kujaribu kumfanya Rais Xi Jinping kupima faida na hasara wa “uhusiano thabiti” na Moscow.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad