Serikali yaingilia kati sakata la GSM, Makonda



Dar es Salaam. Serikali imesema inalichunguza sakata la aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na mfanyabiashara Ghalib Said Mohamed (GSM) la kugombea kiwanja Na.60 kilichopo Regent Estate Manispaa ya Kinondoni jijini hapa.

Akizungumza mwisho wa wiki iliyopita, Wakili wa GSM, Alex Mgongolwa alisema mteja wake ana vielelezo vyote, huku Makonda akimtaka mfanyabiashara huyo kumwachia mali yake.

Akizungumza jana na Mwananchi kwa simu, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Salum Hamduni alisema suala hilo wanalifanyia kazi.

“Uchunguzi upo wa namna nyingi. Na mimi taarifa nimezisikia kupitia vyombo vya habari lakini tunaona kuna kazi ya kufanya katika hilo. Kwa hiyo tumelichukua tunalifanyia kazi,” alisema Hamduni.


 
Akizungumza na gazeti hili kuhusu uhalali wa vielelezo vya wawili hao, Kamishna wa Ardhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Idrisa Kayera alisema vyombo vya Serikali vinavyochunguza suala hilo.

“Zinachunguzwa (hati) na mamlaka nyingine ili kujua uhalali wao. Sisi tukipata wakishatoa maelekezo tutaendelea na hatua nyingine.

“Kwa mujibu wa utaratibu ni kwamba mtu ukifanya uhamisho anatakiwa awasilishe ofisini, ili ijulikane, lakini hilo tumeziachia mamlaka zifanyie kazi ili kujua,” alisema.

Alisisitiza kuwa hizo ni mamlaka za uchunguzi, bila kuzitaja, huku akizitaka pande mbili kwenda kushtaki kwenye vyombo vya Dola.

“Kwa sababu wao wenyewe ndio walihusika kwenye mkataba baina ya Makonda na GSM, wao wapeleke kule, majibu tutaletewa, wakisema hivi vitu havina uhalali tutachukua hatua,” alisema.

Akifafanua zaidi, Kayera alisema GSM alishatoa taarifa idara ya ardhi kuhusu kupotea kwa hati ya kiwanja hicho, na alipewa nakala ya uthibitisho mwingine. “Baada ya kutoa taarifa kuwa amepoteza na kwa mujibu wa sheria, ukipoteza hati unaleta taarifa, inatangazwa kwenye gazeti la kawaida, inatolewa certified, kwa mujibu wa kumbukumbu, hatua hizo zilifuatwa, lakini kwa sasa si rahisi kusema nani ni halali,” alisema.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad