Serikali yamtakia heri Kiduku
SERIKALI imesema ina imani na bondia Twaha Kassim ‘Kiduku’ kuwa atafanya vizuri katika pambano lake lijalo la kimataifa dhidi ya bondia kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Alex Kabangu na kumtakia kila la heri.
Kiduku anatarajiwa kupanda ulingoni Jumamosi hii katika pambano la raundi nane uzito wa kati kuwania mkanda wa Afrika wa UBO litakalofanyika mjini Morogoro.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Yusuph Singo alisema hana wasiwasi na bondia huyo kutokana na uwezo mkubwa alionao atapeperusha vyema bendera ya Tanzania.
“Twaha ni mtu wa kazi wa pambano kubwa, Watanzania twendeni Morogoro tukamuunge mkono bondia huyu, naamini kabisa hatatuangusha, atafanya vizuri na kupeperusha vyema bendera ya nchi,” alisema.
Alisema litakuwa ni pambano lenye ushindani, kwani hata mpinzani wake Kabangu ni mzuri.
“Mabondia wengi wa DRC ni wazuri na wamekuwa wakileta ushindani kwa mabondia wetu,” alisema na kuongeza kuwa ngumi ni miongoni mwa michezo inayopewa kipaumbele kuhakikisha inafanya vizuri sio tu ndani bali hata kimataifa.
Alisema hata michezo ambayo haijapewa kipaumbele ikijitahidi kwa kufanya mashindano yakaonekana itaingizwa katika usaidizi wa serikali hapo baadaye.